1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yangoon. Gambari akutana na Aung San Suu Kyi.

1 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/CBLB

Mjumbe maalum wa umoja wa mataifa Ibrahim Gambari amekutana na kiongozi wa upinzani wa Burma Aung San Suu Kyi, katika juhudi za kupata suluhisho la amani katika ghasia za nchi hiyo.

Wanadiplomasia wamesema kuwa Gambari alikutana na Suu Kyi katika mji mkuu wa nchi hiyo, Rangoon , baada ya kuhudhuria mazungumzo na majenerali wanaotawala nchini humo katika mji ulioko mbali na mji huo mkuu wa Naypyitaw.

Gambari ambaye yuko nchini Burma amesema kuwa hii ni nafasi kwa viongozi wa utawala wa kijeshi kujishughulisha na mazungumzo na upande wa upinzani.

Katibu na mkuu pamoja na mimi binafsi tunajishughulisha na kutoa ujumbe kwa maafisa nchini Myanmar , tukitoa wito wa kujizuwia kwa upande wa maafisa wa serikali kutokana na jinsi wanavyolishughulikia suala la matukio ya hivi karibuni. Lakini muhimu zaidi tunawataka viongozi kuangalia matukio ya hivi karibuni kuwa ni nafasi ya kujishughulisha kwa dhati katika mazungumzo ya kuwajumuisha wale ambao kwa sasa wametengwa na utaratibu mzima wa kisiasa nchini mwao.

Taarifa iliyotolewa na umoja wa mataifa haikusema ni lini Gambari huenda atakutana na jenerali mkuu wa Burma ,Than Shwe.

Katika muda wa wiki moja iliyopita , majeshi ya Burma yamevamia majumba ya watawa wa dini ya Kibudha na kuwakamata na kuwapiga mamia ya watawa pamoja na waandamanaji wengine. Pia waliwafyatulia risasi waandamanaji ambao hawakuwa na silaha. Utawala huo wa kijeshi umesema kuwa watu 10 wameuwawa katika mapambano hayo, ikiwa ni pamoja na mwandishi habari kutoka Japan. Duru huria zinasema kuwa idadi ya watu waliouwawa ni kubwa zaidi.