1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yaya Toure ndiye Mfalme wa soka Afrika

10 Januari 2014

Mchezaji nyota wa Manchester City Yaya Toure ameshinda kwa mara ya tatu mfululizo tuzo ya mchezaji bora barani Afrika. Lakini ushindi huo umekosolewa na maafisa wakuu wa soka nchini Nigeria

https://p.dw.com/p/1AonG
Yaya Toure Manchester City
Picha: Pius Utomi EkpeiI/AFP/Getty Images

Toure mwenye umri wa miaka 31 ambaye ni raia wa Cote d'Ivoire, pia alsinda tuzo hiyo ya Shirikisho la Soka barani Afrika - CAF, mwaka wa 2011 na 2012. John Obi Mikel wa Nigeria, ambaye anachezea klabu ya Chelsea ya Uingereza alikuwa wa pili huku Didier Drogba pia kutoka Cote d'Ivoire akichukua nafasi ya tatu.

Toure alisema "Kwa kweli ilikuwa vigumu sana kushinda. kwa sababu kulikuwa na wapinzani wakali mbele yangu, Obi Mikel, na Didier Drogba, kwa hivyo nilidhani nitashindwa, na sasa nimebahatika na nina furaha kwa mafanikio yangu. Ninapenda kile ninachofanya".

Mchezaji shujaa wa Misri Mohamed Aboutrika alimpiku mwenzake Ahmed Fathy na Sunday Mba wa Nigeria katika kushinda taji la mchezaji bora anayecheza soka lake barani Afrika.

Stephen Keshi, alishinda tuzo ya Kocha bora wa mwaka baada ya kuwaongoza the Super Eagles kushinda kombe la mataifa ya Afrika, na kufuzu katika dimba la kombe la dunia nchini Brazil. Keshi amesema "Kwangu nisingeshinda tuzo hii bila wachezaji wangu, siwezi kufanya pekee yangu, na pia hata bila makocha wasaidizi wangu, na kila mmoja nyuma yangu kufanya kazi kwa bidii, siyo rahisi, kwa hivyo hao ndio walionisaidia kushinda".

Kiungo wa Nigeria, na klabu ya Chelsea John Obi Mikel alikuwa wa pili mbele ya Dider Drogba
Kiungo wa Nigeria, na klabu ya Chelsea John Obi Mikel alikuwa wa pili mbele ya Dider DrogbaPicha: AP

Na muda mfupi baada ya ushindi huo wa Toure, Maafisa wakuu wa soka nchini Nigeria waliukosoa utaratibu uliotumiwa kumpata mshindi. Utaratibu unaotumiwa ni kwamba Makocha wa timu 54 za mataifa wanachama wa CAF huwapigia kura wachezaji 10 wanaoteuliwa, kwa mizani ya pointi moja hadi kumi, huku atakayepata pointi nyingi akipata tuzo hiyo.

Toure alikusanya pointi 373 na akapigiwa kura na makocha 28, na kumpa mchezaji huyo wa Manchester City ya Uingereza ushindi wake wa tatu mfululizo baada ya kunyakua taji hilo mwaka wa 2011 na 2013. Kiungo wa Chelsea Mikel, alikuwa wa pili na pointi 275, huku makocha wanne tu wa timu za taifa akiwemo wa nchi yake Nigeria, wakimpigia kura kama mchezaji bora.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman