Zaidi ya asilimia moja ya jumla ya watu duniani ni wakimbizi
18 Juni 2020Takriban watu milioni 80 kote duniani walilazimika kuyahama makaazi yao kutokana na machafuko na mateso, ikiwa ni idadi kubwa kuwahi kurekodiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi. Syria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya watu waliokimbia makwao kutokana na machafuko.
Idadi hiyo ni zaidi ya asilimia moja ya jumla ya watu duniani ambao ni wakimbizi, wakimbizi wa ndani na wahamiaji. Kamishna mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi, UNHCR, Filippo Grandi ameliambia shirika la habari la Ufarabsa, AFP kwamba kumekuwa na udhaifu katika kushughulikia mizozo duniani.
''Shirika la UNHCR limetoa ripoti kuhusu hali ya wakimbizi mnamo mwaka 2019 na kwa bahati mbaya kwa mara nyingine tena, idadi ya wakimbizi inaendelea kuongezeka kila mwaka toka mwaka wa 2012. Inamaanisha kwamba kuna ongezeko la machafuko ya vita ambayo yalisababisha watu kuyahama makaazi yao''.
Jumuiya ya kimatifa yashindwa kuleta amani duniani
Ripoti ya shirika hilo la kuwahudumia wakimbizi inaelezea kwamba mwaka 2019 kulikuwa na ongezeko la wakimbizi, wakimbizi wa ndani na wahamiaji milioni 9 ukilinganisha na mwaka uliopita.
Grandi anasema kwamba idadi ya wakimbizi duniani imeongezeka mara dufu ukilinganisha na miaka kumi iliopita ambayo ilikuwa jumla ya wakimbizi milioni 40. Anasikitishwa kuona jumuiya ya kimataifa inaendelea kugawanyika, na kushindwa kuhakikisha amani, hali ambayo inaleta wasiwasi wa ongezeko zaidi la wakimbizi mwaka ujao wa 2021.
Ripoti hiyo inaonyesha kwamba mnamo mwaka 2019, watu milioni 46 walikuwa wakimbizi wa ndani, na wengine 26 milioni walikimbilia nje ya mipaka ya nchi zao. Watu wengine milioni 4.2 walikuwa wahamiaji na Venezuala pekee ilirekodi wakimbizi milioni 3.6. Mwaka jana kuliripotiwa watu milioni 11 waliokimbia makwao kote duniani kutokana hasa na machafuko ya kivita.
Nchini Syria baada ya miaka 9 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, watu milioni 13.2 waliyahama makaazi yao na kukimbilia maeneo mengine ndani ya nchi hiyo.
Asilimia 68 ya jumla ya wakimbizi duniani ni kutoka nchi tano ambazo ni Syria, Venezuela, Afganistan, Sudan Kusini na Myanmar. Filippo Ghandi ameiomba jumuiya ya kimataifa kuwa na umoja na kwa lengo la kuwa na nia nzuri ya kisiasa ili kusuluhisha mizozo kwenye nchi hizo.
''Tunashuhudia ongezeko kubwa la umasikini. Vizuwizi kutokana na janga la virusi vya corona vinaathiri aina ya uchumi ambao wakimbizi hao walikuwa wanategemea zaidi, uchumi usio rasmi, malipo ya kila siku kutokana na kazi ya rejareja. Hivi sasa kila kitu kimeondoka kutokana na hatua za kutotoka nje''.
Msaada zaidi wahitajika kwa ajili ya Wakimbizi
Ripoti hiyo haikujumuisha hali ya wakambizi kutokana na janga la virusi vya corona. Grandi amesema kwamba kutokuweko na msaada muhimu kwa wakimbizi hao pamoja na jamii zinazowahifadhi, kunaweza kusababisha uwepo wa wakimbizi zaidi.
Grandi pia alizikosoa serikali zinazowafungia mipaka wakimbizi na wahamiaji. Huku akiziomba nchi kuwahakikishia watu haki za uhamiaji licha ya kufungwa kwa mipaka na hatua za kutotoka nje.
Mkuu wa shirika hilo la kuwahudumia wakimbizi amesema shughuli pekee ambazo hazikujali janga la virusi vya corona ni vita, mizozo na umwagikaji damu ambao uliendelea na hilo kwa bahati mbaya limesababisha watu kutolijali janga hilo kwa sababu maisha yao yako hatarini.