1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zambia kufunga mpaka wake na Tanzania kufuatia corona

Mwandishi: Hawa Bihoga/Dar es salaam11 Mei 2020

Baada ya Zambia kutangaza kufunga mpaka wake kwa muda na Tanzania, wachambuzi wa masuala ya kidiplomasia wanasema kuna umuhimu wa mataifa hayo mawili kufanya mazungumzo za pamoja ili kukabiliana na janga la corona.

https://p.dw.com/p/3c19J
Sambia Lusaka Präsident Edgar Chagwa Lungu
Picha: Getty Images/AFP/S. Dawood

Hadi sasa mamlaka nchini Zambia imethibitisha visa vya maambukizi ya virusi vya corona takriban 76, ikiwa ni sehemu ya kuzuia maambukizi kuendelea kusambaa nchini humo, na imeamua kufunga mji wa Nakonde ambao upo kwenye mpaka kati ya nchi hiyo na Tanzania, kwa siku zisizopungua saba.

Akizungumza na wanahabari kwa niaba ya Rais Edgaer Lungu waziri wa afya nchini humo Chitalu Chilufya amesema amri hiyo inayoanza leo ya kufunga mpaka wa Nakonde kwa upande wa Zambia ambao ni jirani na Tunduma kwa Tanzania  itatoa fursa kwa utekelezwaji wa mikakati mipya ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.

Itakumbukwa kuwa itifaki ya nchi zilizo ndani ya jumuia ya maendeleo kusini mwa Afrika SADC katika kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona inaonesha, kila taifa litaendelea kukabiliana na maambukizi ya virusi vya hivyo kwa kuzingatia miongozo ya kimataifa kadhalika hali halisi ya mataifa hayo, lakini pia usafirishaji wa bidhaa muhimu utaendelea kuzingatiwa katika nchi wananchama.

Katika hatua hii wachambuzi wa masuala ya diplomasia za kimataifa wanasema kuwa, kuna haja ya kufanyika kwa mazungumzo baina ya nchi hizo, kwani kutekeleza kwa agizo kufunga mpaka ni kwenda kinyume na makubaliano ya SADC ambayo yaliafikiwa na baraza la mawaziri hivi karibuni. Abbas Mwalimu ambaye ni mchambuzi wa diplomasia za kimataifa amesisitiza, kuwa suluhisho si kufunga mpaka huo muhimu kwa uchumi wa mataifa hayo yalio kusini mwa Afrika.

Zambia imethibitisha visa 76 vya maambukizi ya corona.
Zambia imethibitisha visa 76 vya maambukizi ya corona.Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Mwiche

Aidha uamuzi wa huu wa serikali ya Rais Edgar Lungu unatajwa kuwaathiri pakubwa wafanyabiashara pamoja na watoa huduma ya usafirishaji wa mizigo baina ya mataifa hayo mawili kwani zaidi ya magari ya mizigo elfu kumi na tano hufanya shughuli zake za usafirishaji kati ya nchi hizo mbili.

Makamu wa Rais wa chama cha usafirishaji mizigo nchini TanzaniaOmary Kiponza ameiambia DW kuwa miongoni mwa hasara zitakazoshuhudiwa ni pamoja na kufurika kwa mizigo katika badari ya Dar es salaam ambayo Zambia inaitumia kwa kiwango kikubwa.

Jumuia mbalimbali za kimataifa zimekuwa zikiishutumu wazi serikali ya Tanzania kwa kile walichokitaja kushindwa kushughulikia ipasavyo tatizo la corona, hatua ambayo inatajwa na wachambuzi wa mambo kuwa baadhi ya nchi kwa jumuia ya Afrika Mashariki na SADC kuchukua uamuzi wa kuweka vizingiti kwa watu wanaotoka katika nchi hiyo.