Zambia na Cote d'ivoire kuumana katika fainali
9 Februari 2012Zambia waliizuia fainali ambayo wengi walitaraji kuiona kati ya Ghana na Cote d'ivoire wakati walipowaduwaza The Black Stars kwa goli moja kwa nunge, kufuatia bao lake Emmanuel Mayuka, huku nao Cote d'ivoire wakiwachapa Mali kwa goli hilo moja kupitia kazi safi yake Gervinho aliyefunga bao katika kipindi cha kwanza.
Mechi hiyo iliyochezwa katika mji mkuu wa Gabon Libreville, iliegemea upande mmoja huku The Elephants wa Cote d'ivoire, wakigonga chuma cha lango la Mali mara mbili katika dakika 15 za mwanzo. Nahodha Didier Drogba na Yaya Toure hawakuwa na bahati kufunga baada ya juhudi zao kugonga mwamba.
Gervinho alifunga bao la ustadi
Jambo la kushangaza ni kuwa iliwachukua Cote d'ivoire dakika 45 kuchukua uongozi. Bao hilo lilifungwa naye mshambulizi wa Arsenal Gervinho, ambaye aliupokea mpira katikati mwa uwanja na akakimbia nao kabla ya kumbwaga kipa wa Mali Soumaila Diakite na kutikisa wavu.
Cote d'ivoire iliendela kuizidi nguvu Mali katika kipindi cha pili lakini hakuna bao jingine lililopatikana, huku Drogba akikosa nafasi ya wazi. Mali ambao walikuwa wakiitafuta fainali yao ya pili katika kinyang'anyiro hicho, waliwasukuma wachezaji wake mbele kutafuta bao la kusawazisha lakini wakashindwa kumsumbua kipa wa Cote d'ivoire Boubacar Barry, ambaye hajafungwa bao hata moja katika dimba hili kufikia sasa. Baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa, wachezaji wa Cote d'ivoire walikimbia uwanjani na kusheherekea ushindi huo uliowapeleka katika fainali yao ya tatu.
Zambia watashiriki fainali yao ya tatu katika tamasha hilo la bara la Afrika, baada ya kushiriki kwa mara ya mwisho mwaka wa 1994. Fainali ya Jumapili itakuwa mjini Libreville, ambako timu ya taifa ya Zambia iliangamia mnamo mwaka wa 1993 wakati ndege iliyokuwa ikiwasafirisha kwa mchuano wa kombe la dunia ilipoanguka majini mita 500 kutoka mji huo mkuu wa Gabon na kuwauwa wote waliokuwa ndani:
Asamoah Gyan alipoteza penalti
Mbele ya mashabiki wachache mjini Bata, nchini Guinea ya Ikweta, timu zote mbili zilikosa nafasi za wazi za kufunga bao katika kipindi cha kwanza. Asamoah Gyan wa Ghana alishindwa kufunga mkwaju wa penalty ambao ulizuiwa na kipa wa Zambia Kennedy Mweene na kisha vijana hao wa Black Stars wakamaliza mchezo na watu kumi uwanjani baada ya Derek Boateng kufurushwa uwanjani alipoonyeshwa kadi ya pili ya njano katika dakika ya 84.
Dakika kumi baada ya kipindi cha pili kuanza, Christopher Katongo alipewa pasi safi na Rainford Kalaba lakini nahodha huyo wa Zambia akashindwa kuona lango. Kisha mambo yakaharibika kwa upande wa Black Stars baada ya Mayuka kuwapa Chipolopolo uongozi katika dakika ya 78 kwa kusukuma kimyani bao la ustadi.
Hivyo Ghana na Mali zitakabana koo siku ya Jumamosi (11.02.2012) mjini Malabo, ili kumtafuta mshindi wa nafasi ya tatu kabla ya fainali kusakatwa Jumapili (12.02.2012) mjini Libreville.
Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Yusuf, Saumu