Zambia: Rais Edgar Lungu akubali kushindwa
16 Agosti 2021Rais mteule Hakainde Hichilema katika hotuba yake ya kwanza kwa taifa saa kadhaa baada ya kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa rais, ameulaumu utawala wa Zambia uliokuwepo na ameahidi kuleta demokrasia ya kweli nchini humo. Akiongea muda mfupi baada ya mtangulizi wake Edgar Lungu kukubali kushindwa, alisema yeye na wafuasi wake waliteseka kwenye mikono ya serikali ya kikatili inayoondoka lakini ameahidi kwamba ataikuza demokrasia, utawala wa sheria, kurejesha utulivu na kwamba serikali yake itaheshimu haki za binadamu na uhuru. Hichilema amesema mabadiliko yametokea nchini Zambia.
Pamoja na hayo Hichilema amewahimiza Wazambia kuweka kando migawanyiko na amelaani vurugu na uporaji wa mali, baada ya duka kubwa lililopewa jina la rais Edgar Lungu kuvamiwa na kuporwa.
Hii ni mara ya tatu kwa chama tawala kushindwa na upinzani kwenye uchaguzi nchini Zambia tangu taifa hilo lijipatie uhuru wake kutoka kwa waingereza mnamo mwaka 1964. Yaliyotokea Zambia yanadhihirisha kuimarika kwa demokrasia ya nchi hiyo.
Hata hivyo baada ya shangwe kumalizika, Hichilema aliyekuwa meneja mkuu kwenye kampuni ya mahesabu kabla ya kuingia katika siasa atapaswa kuweka mkazo katika kuufufua uchumi uliozorota. Zambia ilikuwa nchi ya kwanza barani Afrika kushindwa kulipa madeni yake ya kimataifa mnamo mwezi Novemba mwaka uliopita. Kushindwa huko kulisababishwa na kuanguka kwa bei za bidhaa zake inazouza nje na hivyo kuitumbukiza Zambia kwenye mdororo wa uchumi hata kabla ya janga la corona lililoifanya hali iwe mbaya zaidi.
Wakati huo huo hati fungani za Zambia ziliongezeka thamani kwa karibu senti 2 za dola baada ya kutangazwa ushindi wa Hichilema. Sarafu ya Zambia ya kwacha pia imeimarika kwa karibu asilimia 1% dhidi ya dola.
Vyanzo://AFP/RTRE