Zambia yapigwa kumbo AFCON 2013
30 Januari 2013Zambia ilitoka sare tasa jana dhidi ya Burkina Faso, ambayo imefuzu kuingia robo fainali ya mashindano ya mwaka huu, AFCON 2013, kwenye mechi iliyochezwa katika uwanja wa Mbombela nchini Afrika Kusini. Sare ya tatu kwa Chipolopolo haikutosha kuiwezesha kusonga mbele katika mashindano hayo.
Timu ya mwisho iliyoshinda kombe la mataifa ya Afrika na kushindwa kusonga mbele katika duru ya pili kwenye mashindano yaliyofuata ni Algeria mnamo mwaka 1992.
Burkina Faso imeongoza katika kundi C na kuweka historia yake, huku ikifuzu kwa raundi ya pili kwa mara ya kwanza katika nchi ya kigeni. Burkina Faso imewahi kusonga mbele katika mashindano ya kuwania kombe la mataifa Afrika, mara moja tu wakati ilipoyaandaa mnamo mwaka 1998.
Kocha wa Burkina Faso, raia wa Ubelgiji, Paul Put, amesema anadhani huu ni ufanisi mkubwa kabisa wa timu ya nchi hiyo kwa kuwa iliwahi kuyaandaa mashindano hayo mara moja na ikafaulu kufika nusu fainali. "Lengo letu la kwanza tulitaka kufanya vyema zaidi kuliko mashindano ya hivi karibuni ya kombe la mataifa ya Afrika na tulikuwa tumefanikiwa kwa kutoka sare dhidi ya Nigeria na Ethiopia. Nadhani ni historia kwa Burkina Faso," akaongeza kusema kocha Put.
Zambia haikung'ara
Kocha wa Zambia, Herve Renard, amebakia kuwa mwingi wa matumaini na mwanafalsafa. "Ni bora uwe umeshinda kitu katika maisha yako, kuliko kuingia robo fainali kila mara lakini usifaulu kushinda chochote," amesema kocha huyo na kuongeza kusema, "Huu sio mwisho wa dunia. Zamani tulikuwa tukirudi nyumbani mara nyingi baada ya raundi ya kwanza, na leo lazima tukubali kwamba huu ni mchezo wa soka."
Zambia haikuonyesha mchezo mzuri na mshambuliaji wake matata, Collins Mbesuma, alikosa nafasi kadhaa za kuutikisa wavu wa Burkina Faso. Kwa upande wao Burkina Faso walifahamu walihitaji sare tu kuweza kufuzu na waliridhika kucheza katikati mwa uwanja ili kupunguza kasi ya mchezo huo, hususan baada ya kumpoteza kipa wao mahiri, Alain Traore, kutokana na jeraha alilolipata dakika ya 10 ya mtanange huo.
"Viungo vya leo ilikuwa ni pilipili nyingi na chumvi kidogo kwenye mchuzi," ndivyo alivyotamka kocha wa Burkina Faso, Paul Put.
Zambia ilipata changamoto kubwa kutokana na hali ya uwanja wa Mbombela kuwa na mchanga mwingi. Kocha wa Chipolopolo, Renard, amesema, "Nikiulaumu uwanja basi watu watasema nalia, lakini nadhani baada ya mkutano huu na waandishi wa habari unahitaji tu kwenda uwanjani na ujionee kama inawezekana kucheza kandanda safi."
Nigeria yaitwanga Ethiopia
Kwenye mechi nyengine ya kundi C, Nigeria iliinyoa Ethiopia bila maji kwa kuitandika mabao 2-0 katika uwanja wa mjini Rustenburg. Kocha wa Nigeria, Stephen Keshi, amesema, "Ushindi huu ni wa Wanigeria wote popote walipo ulimwenguni. Huu ni wakati wa kushangilia."
Ushindi wa Nigeria dhidi ya Ethiopia umewatia tumbo joto wachezaji huku wakisubiri kuvaana na Cote d'Ivoire kwenye robo fainali. Burkina Faso inasubiri kukwaana na mshindi wa mechi ya kundi C kati ya Togo na Tunisia mjini Nelsprut itakayochezwa baadaye leo. Ethiopia na Zambia wanafunganya virago na kuelekea uwanja wa ndege tayari kurejea nyumbani.
Mwandishi: Josephat Charo/APE/AFPE
Mhariri: Hamidou, Ummilkheir