Zelenskiy ataka dunia isiiuzie Urusi vifaa vya makombora
15 Juni 2023Haya yanafanyika wakati ambapo ujumbe wa amani wa Afrika unaojumuisha marais sita, unafunga safari kuelekea Ukraine Alhamis kushiriki juhudi za upatanishi kati ya Kyiv na Moscow.
Taarifa iliyotolewa na serikali ya Ukraine Alhamis imesema makombora mengine matatu yameshambulia miundombinu ya viwanda katika eneo la Dnipropetrovsk mashariki mwa Ukraine.
Taarifa hiyo imetolewa muda mfupi baada ya gavana wa eneo la Crimea aliyepewa mamlaka na Urusi kusema kwamba majeshi ya Urusi, yamedungua ndege 9 zisizokuwa na rubani katika eneo lake bila kusababisha vifo.
Dunia yastahili kufunga njia za kusambaza vifaa vya makombora Urusi
Mwanzoni mwa wiki Rais wa Urusi Vladimir Putin, alisema kwamba majeshi ya Urusi yanawasababishia hasara kubwa wanajeshi wa Ukraine.
Rais Volodymyr Zelenskiy wa Ukraine kwa upande wake ametoa wito wa mataifa duniani kutoiuzia Urusi vifaa vya kutengeza makombora yake.
"Sehemu kubwa ya vifaa vya makombora ya Kalibr vilipelekwa Urusi kutoka nchi zengine. Bila shaka, kila njia ya kusambaza vifaa hivi ni njia ya kuutia nguvu ugaidi. Dunia ina njia za kukata njia hizo kutoka kila nchi, kutoka kila kampuni ambayo vifaa vyake vinatumika na watengezaji makombora wa Urusi," alisema Zelenskiy.
Wakati huo huo, shirika la habari la Urusi TASS, limesema mtoto mmoja ameuwawa kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na Ukraine katika eneo la kusini mwa Ukraine la Kherson ambalo sehemu yake inashikiliwa na Urusi.
Haya yanajiri wakati ambapo gazeti la nchini Zambia la Lusaka Times limeripoti kuwa ujumbe wa marais sita wa Afrika utakutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy hapo kesho na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin mnamo siku ya Jumamosi.
Ripoti kutoka Uganda zinaarifu Rais Yoweri Museveni amesema marais wa Misri, Visiwa vya Comoros, Afrika Kusini, Senegal, Kongo Brazzaville na Zambia watawasili nchini Poland na kuabiri treni kuelekea Kyiv baadae leo.
Museveni ambaye alikuwa sehemu ya ujumbe huo wa amani wa marais wa Afrika hatokuwa miongoni mwa viongozi hao kwa kuwa aliambukizwa Uviko-19 na sasa atawakilishwa na mjumbe wa Uganda nchini Poland.
Mkuu wa IAEA aelekea Zaporizhzia licha ya mapigano
Kwengineko Shirika la habari la urusi la TASS limeripoti kuwa mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki IAEA Rafael Grossi, amevuka kizuizi cha barabarani cha Urusi katika eneo la Zaporizhzia huko Ukraine kunakoendelea mapigano makali, akiwa njiani kukizuru kinu cha nyuklia cha Zaporizhzia.
Ziara hiyo ya Grossi ilistahili kufanyika Jumatano ila ikaahirishwa kutokana na sababu za kiusalama kwa kuwa Urusi na Ukraine ziliripoti mapigano makali mno kusini mwa Ukraine.
Mkuu huyo wa IAEA mwanzoni mwa wiki akiwa mjini Kyiv, alisema, anahofia kwamba kinu hicho kinaweza kushambuliwa katika mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Ukraine wakati ikijaribu kuyarudisha tena katika himaya yake maeneo yaliyotwaliwa na Urusi.
Vyanzo: Reuters/DPA/AFP