Zelensky ahofia mashambulizi makali zaidi Siku ya Uhuru
21 Agosti 2022"Urusi inaweza kujaribu kufanya kitu fulani makhsusi kabisa cha kuogofya, makhsusi kabisa cha kikatili," alisema Zelensky kwenye hotuba yake ya kila siku, usiku wa Jumamosi (20 Agosti).
"Moja ya malengo makuu ya adui ni kutudhalilisha," na "kupandikiza hisia za mashaka, wasiwasi na mgogoro" lakini "tunapaswa kuwa na ushujaa wa kutosha kukabiliana na uchokozi huu wote" na "kuwafanya wavamizi kulipia gharama ya ugaidi wao," alisema.
Siku ya Uhuru wa Ukraine hapo Jumatano (Agosti 24) pia itakuwa siku ya kukumbuka miezi sita tangu Urusi kuivamia sehemu hiyo ya zamani ya jamhuri ya Kisovieti.
Kumekuwa na wasiwasi kwamba Urusi itatumia siku hiyo kuwashitaki hadharani wapiganaji wa Ukraine waliotekwa wakati mji wa bandari wa Mariupol ulipozingirwa.
Mshauri wa rais, Mykhaylo Podolyak, alisema kwamba Urusi inaweza kuongeza mashambulizi yake ya kijeshi siku hiyo.
"Urusi ni dola la kale ambalo linafungamanisha matendo yake na tarehe maalum, ni aina fulani ya imani ya ndani," shirika la habari la Interfax-Ukraine lilimnukuu akisema.
"Wanatuchukia na watajaribu kuongeza idadi ya mashambulizi ya mabomu kwenye miji yetu ukiwemo Kyiv wakitumia makombora kutokea baharini," alisema Podolyak.
Marufuku ya kutotoka nje
Mamlaka za Kyiv zilisema siku ya Jumamosi kwamba mikusanyiko yote ya umma imepigwa marufuku kutokea tarehe 22 hadi 25 Agosti.
Katika mji wa kaskazini mashariki wa Kharkiv, gavana wa huko alitangaza marufuku ya kutotoka nje kuanzia jioni ya tarehe 23 Agosti hadi asubuhi ya tarehe 25 Agosti.
"Hatutaruhusu aina yoyote ya uchokozi wa adui. Kuweni na tahadhari kadiri iwezekanavyo wakati wa sikukuu ya uhuru wetu," aliandika gavana Oleg Synegubov kwenye mtandao wa Telegram.
Kharkiv imekuwa ikishambuliwa kwa wiki nzima kwa mabomu ya Urusi na siku ya Jumapili (Agosti 21), mamlaka za huduma ya uokozi zilisema mwanamke mmoja aliuawa na raia wengine wengine kujeruhiwa kwenye mashambulizi ya anga ya usiku wa kuamkia siku hiyo.
Raia wanne waliripotiwa kuuawa kutokana na mashambulizi ya Donestk, alisema gavana anayeelemea upande wa Kyiv, Pavlo Kyrylenko.
Makombora matano yalirushwa kutoka Bahari Nyeusi kuelekea mji wa Odessa, alisema msemaji wa jimbo hilo. Mawili yalidunguliwa na mfumo wa ulinzi wa anga na matatu yalipiga eneo tupu bila kusababisha madhara yoyote.
Jeshi la Ukraine lilisema kupitia mtandao wa Facebook kwamba majeshi ya Urusi yanashikilia sehemu ya mji wa Blagodatne ulio kusini mwa mkoa wa Mykolaiv.