1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

Zelensky aonyesha utayari wa kubadilishana wafungwa na Urusi

13 Januari 2025

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema yuko tayari kuwarejesha nchini mwao wanajeshi wawili wa Korea Kaskazini waliotekwa, kwa mabadilishano ya kuachiliwa huru wafungwa wa kivita raia wa Ukraine walioko Urusi.

https://p.dw.com/p/4p5F6
Ubelgiji | Brussels | EU
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Remko de Waal /ANP/IMAGO

Pendekezo la Zelensky amelitoa saa chache baada ya idara ya kitaifa ya ujasusi ya Korea Kusini kuthibitisha tangazo la siku iliyopita kwamba Ukraine imewakamata wanajeshi wawili wa Korea Kaskazini.

Mamlaka nchini Ukraine siku ya Jumamosi ilisema wanajeshi hao wawili walijeruhiwa vibaya katika uwanja wa vita wakati wakipambana na wanajeshi wa Ukraine katika eneo la Kursk nchini Urusi, lakini wakati huo hawakutoa ushahidi kuthibitisha uraia wao.

Soma pia: Urusi yadai kuviteka vijiji viwili mashariki mwa Ukraine

Hata hivyo, jana Jumapili, Idara ya ujasusi ya Korea Kusini NIS imeliambia shirika la habari la AFP kwamba, imethibitisha kuwa jeshi la Ukraine limewakamata wanajeshi wawili wa Korea Kaskazini mnamo Januari 9 katika uwanja wa vita eneo la Kursk, nchini Urusi.

Kursk | Ukraine | Korea Kaskazini
Mmoja wa mwanajeshi wa Korea Kaskazini aliyekamatwa na jeshi la Ukraine Januari 11, 2025.Picha: Anadolu/picture alliance

Zelensky ameandika katika mtandao wa kijamii wa X kwamba wanajeshi wa Korea Kaskazini ambao hawataki kurudi nyumbani na wanaoonyesha nia ya kuleta amani kwa kueleza ukweli kuhusu vita hivyo nchini mwao, watapewa kile alichokiita "fursa nyengine."

Alipoulizwa mwaka jana kuhusu ushiriki wa wanajeshi wa Korea Kaskazini, Rais wa Urusi Vladimir Putin hakukiri wala kukanusha kwamba nchi hiyo inatumia wanajeshi wa Korea Kaskazini katika vita vyake dhidi ya Ukraine.

Soma pia: Wanajeshi wa Korea Kaskazini wakamatwa na Ukraine

Ukraine, Marekani na Korea Kusini zimeishtumu Korea Kaskazini, nchi yenye silaha za nyuklia kwa kutuma wanajeshi zaidi ya 10,000 kulisaidia jeshi la Urusi katika vita vyake dhidi ya Ukraine.

Nchi hizo – Urusi na Korea Kaskazini, zimeimarisha ushirikiano wao wa kijeshi tangu Moscow ilipoivamia Ukraine mwaka 2022.

Marekani yasema Korea Kaskazini imetuma wanajeshi 10,000 Urusi

Ikulu ya Marekani White House imesema idadi kubwa ya wanajeshi wa Korea Kaskazini wameuawa vitani.

Mnamo mwezi Disemba, shirika la ujasusi la Korea Kusini liliripoti juu wa kukamatwa kwa mwanajeshi wa kwanza wa Korea Kaskazini na vikosi vya Ukraine japo baadaye alifariki dunia.

Mwaka mmoja tangu Urusi kuivamia Ukraine

"Hakuna shaka yoyote duniani kwamba jeshi la Urusi linategemea msaada wa kijeshi kutoka Korea Kaskazini," amesema Zelensky.

Rais huyo wa Ukraine amechapisha video inayoonyesha wanajeshi wawili wa Korea Kaskazini waliotekwa wakihojiwa. Mmoja anaonekana amelala kwenye kitanda huku mwengine akiwa ameketi kitandani na bandeji shingoni.