Zelensky atembelea wanajeshi mstari wa mbele wa vita
20 Desemba 2022Msemaji wa rais huyo wa Ukraine, Serhii Nykyforov, alisema Zelensky aliutembelea mji unaowaniwa wa Bakhmut mashariki mwa Ukraine siku ya Jumanne (Disemba 20), ambako aliwatunikia zawadi na medali wanajeshi hao walio mstari wa mbele wa mapambano.
Katika hotuba yake ya usiku wa Jumatatu kwa taifa, Zelensky aliuelezea mji huo kuwa "eneo tete" katika ukanda wote ulio mstari wa mbele wa mapambano wenye urefu wa kilomita 1,300. Miezi kadhaa nyuma, alikuwa amesema jeshi la Urusi liliugeuza mji huo kuwa mabaki matupu.
Ingawa rais huyo hajawahi kuondoka nchini Ukraine tangu Urusi kuanza uvamizi wake miezi kumi iliyopita, lakini amekuwa akitembelea maeneo yenye mapigano kuonesha uungaji mkono wake kwa wanajeshi mara kwa mara.
Kiev iko hali mbaya
Hayo yakijiri, kazi ya matengenezo inaendelea katika maeneo kadhaa ya mji mkuu wa Ukraine, Kiev, ambayo yameshuhudia uharibifu mkubwa wa miundombinu kutoka na mashambulizi ya ndege zisizo rubani za Urusi.
Mbali na kukosa maji na umeme kutokana na mashambulizi hayo, Meya Vitali Klitschko wa mji huo alisema hata usafiri wa treni ulipaswa kusitishwa kwa muda kutokana na maharibiko makubwa kwenye mfumo wake wa kusambazia umeme.
Katika baadhi ya mitaa, wakaazi wake wanakabiliana na wakati mgumu zaidi kutokana na kukosekana kwa njia za kupashia joto nyumba zao, wakati huu msimu wa baridi kali ukiendelea.
Klitschko alisema hapo jana kwamba kutokana na mashambulizi hayo ya ndege zisizo rubani za Urusi, wanaweza asilimia 50 tu ya umeme, huku nakisi ikiwa zaidi ya asilimia 30.
Putin abadilisha mkakati
Wakati huo huo, taarifa kutoka idara ya ujasusi ya Uingereza imesema Rais Vladimir Putin wa Urusi anajaribu kurejesha hamasa ya vikosi vyake vilivyorudishwa nyuma kutoka mstari wa mbele wa mapambano.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Wizara ya Ulinzi wa Uingereza imesema ziara ya Putin kwenye Makao Makuu ya Operesheni Maalum ya Kijeshi iliyofanyika hivi karibuni ilikuwa ni sehemu ya mkakati huo. Katika ziara hiyo, Putin aliandamana na Mkuu wa Majeshi Valey Gerasimov na Waziri wa Ulinzi Sergei Shoigu.
Wizara hiyo ya ulinzi ya Uingereza imedai kwamba mkutano huo wa Putin "ulidhamiria kuonesha wajibu wa pamoja kwenye operesheni maalum ya kijeshi nchini Ukraine, na hivyo kumuondosha Putin kwenye lawama za moja kwa moja juu ya kurudishwa nyuma majeshi ya Urusi, idadi kubwa vifo vya wanajeshi hao, na kupanda kwa hasira miongoni mwa raia."