Zelensky asema kuna taifa la kigaidi ndani ya G20
16 Novemba 2022Akizungumza Jumatano kwa njia ya video katika mkutano wa kilele wa G20, Zelensky ameishutumu Urusi kwa shambulizi la kombora nchini Poland ambalo limewaua watu wawili na ameliita shambulizi hilo kama ''taarifa ya kweli iliyoletwa na Urusi katika mkutano huo''. Zelensky amehimiza kukomeshwa kwa vita, huku akitoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka kujibu shambulizi la Poland.
Zelensky amefanya haraka kuinyooshea kidole cha lawama Urusi, ambayo siku ya Jumanne ilifanya mashambulizi kadhaa nchini Ukraine na kuacha mamilioni ya kaya bila umeme. Rais huyo wa Ukraine ameuhutubia mkutano wa G20 kwa mara ya pili, lakini viongozi kadhaa tayari wameshaondoka katika kisiwa cha Bali nchini Indonesia, miongoni mwao akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov ambaye aliondoka Jumanne.
Viongozi wa G20 wakutana kwa dharura
Zelensky amehutubia muda mchache baada ya viongozi wa mataifa ya Magharibi kufanya kikao cha dharura pembezoni mwa mkutano wa G20, ambako wametoa wito wa kutofikia hitimisho lolote kuhusu eneo ambako kombora hilo limetokea. Mazungumzo hayo yamefanyika baada ya Rais wa Poland, Andrzej Duda kusema kuwa hakuna ushahidi wa wazi kuhusu nani aliyerusha kombora hilo lililotokea katika kijiji cha Przewodow kilichoko kusini mashariki karibu na mpaka wa Ukraine. Duda amesema pia kuwa huenda kombora hilo limetengenezwa Urusi.
Rais wa Marekani, Joe Biden amesema huenda kombora hilo halijarushwa kutoka Urusi. Biden aliyezungumza kwa njia ya simu na Rais Duda, amesema nchi yake itatoa msaada kamili katika uchunguzi wa Poland. Biden ambaye alikutana na viongozi wa Jumuia ya Kujihami ya NATO na kundi la nchi tajiri duniani la G7, amesema amewaeleza viongozi hao kuhusu mazungumzo yake na Duda pamoja na Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg.
''Tumekubaliana kuisaidia Poland katika uchunguzi wa shambulizi hilo karibu na mpaka wa Ukraine. Na nitahakikisha tunajua hasa kilichotokea. Pia tunatoa salamu zetu za pole kwa mauaji ya watu hao wawili. Kisha tutaamua kwa pamoja hatua yetu inayofuata wakati uchunguzi unaendelea,'' alisema Biden.
Aidha, Biden na Duda pia wamekubaliana kuendelea kuwasiliana kwa karibu ili kufahamu hatua zinazofuata wakati uchunguzi ukiendelea.
Scholz aonya kuhusu hitimisho la haraka
Naye Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz ameonya dhidi ya kupata hitimisho la haraka kwenye shambulizi la kombora la Poland na ametoa wito wa kufanyika uchunguzi makini. Akizungumza Jumatano na waandishi habari katika mkutano wa G20 nchini Indoesia, Scholz amesema shambulizi hilo lazima lichunguzwe, sehemu za roketi zinapaswa kuchunguzwa na kisha wasubiri matokeo yake kabla hayajatolewa hadharani.
Ama kwa upande mwingine, viongozi hao wa G20 wamekosoa vikali uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na kuitaka Urusi iwaondoe mara moja wanajeshi wake. Hayo ni kulingana na matakwa yaliyomo kwenye rasimu ya azimio iliyopitishwa mwishoni mwa mkutano wao wa siku mbili.
Huku hayo yakijiri, mabalozi kutoka nchi 30 wanachama wa NATO wanakutana Jumatano mjini Brussels, Ubelgiji kwa mkutano wa dharura baada ya Poland kusema kwamba kombora lililotengenezwa Urusi limeangukia katika ardhi yake na kuwauwa watu wawili.
(AFP, DPA, Reuters)