Zelensky: UN ihakikishe usalama wa kinu cha nyuklia
18 Agosti 2022Zelensky ameitoa kauli hiyo Alhamisi baada ya kukutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres katika mji wa Lviv, Ukraine. Zelensky ameutaka umoja huo kuhakikisha majeshi yanaondolewa katika kinu hicho ili kiweze kukombolewa kabisa kutoka mikononi mwa majeshi ya Urusi.
Kiongozi huyo wa Ukraine pia amekosoa mashambulizi aliyoyataja kuwa ya ''makusudi'' yanayofanywa na Urusi katika kinu hicho. Urusi na Ukraine zimekuwa zikitupiana lawama ya kukishambulia kinu hicho cha nishati ya nyuklia ambacho Urusi ilikidhibiti mwezi Machi.
Viongozi hao wazungumzia pia usafirishaji nafaka
Shirika la habari la Uturuki, Anadolu limeripoti kuwa Guterres alikutana na Zelensky pamoja na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan katika mji wa Lviv. Viongozi hao pia walijadiliana kuhusu usafirishaji wa nafaka, mpango uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa na Uturuki. Zelensky na Guterres pia walizungumzia kuhusu kuachiliwa huru kwa wanajeshi na madaktari walioshikiliwa mateka na Urusi.
Umoja wa Mataifa na Uturuki zina matumaini kwamba mkutano huo wa kilele wa pande tatu utaongeza juhudi kuelekea kupatikana kwa suluhisho la kisiasa katika mzozo wa Ukraine, ambako uvamizi wa Urusi umekuwa ukiendela kwa karibu nusu mwaka sasa.
Wakati huo huo, wizara ya mambo ya nje ya Urusi Alhamisi ilipuuzilia mbali pendekezo la Guterres la kuondoa jeshi lake katika eneo linalozunguka kinu cha nishati ya nyuklia cha Zaporizhzhia kinachodhibitiwa na Urusi, kilichopo kusini mwa Ukraine. Katika mkutano na waandishi habari, msemaji wa wizara hiyo, Ivan Nechaev amesema mapendekezo hayo ''hayakubaliki''.
''Ili kuzuia janga lisitokee kwenye kinu cha nyuklia, ni muhimu kwa vikosi vya Ukraine kuacha kukishambulia kwa makombora. Tunatarajia kwamba wataalamu wa Shirika la Kimataifa la kudhibiti matumizi ya Nishati ya Nyuklia, IAEA watatembelea Zaporizhizhia katika siku zijazo. Tulikubaliana ziara hiyo ifanyike mwezi Juni, lakini ilifutwa na uongozi wa Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa,'' alifafanua Nechaev.
Guterres alitoa pendekezo hilo Agosti
Mapema mwezi huu, Guterres alitoa wito wa kuondolewa kwa wanajeshi na vifaa vya kijeshi katika kinu cha Zaporizhzhia na kuwa na eneo salama kuzunguka kinu hicho.
Ama kwa upande mwingine, wizara ya ulinzi ya Uturuki imesema kuwa jumla ya tani 622,000 za nafaka zimesafirishwa kwa meli kutoka katika bandari za Ukraine kupitia Bahari Nyeusi, baada ya makubaliano yaliyofikiwa mwezi Julai.
Meli 25 zimeondoka katika bandari za Ukraine kuanzia Agosti Mosi. Meli hizo zinapaswa kukaguliwa na timu ya wataalamu wa kimataifa katika kituo cha uratibu wa pamoja kilichoko Istanbul, Uturuki ambacho kimeundwa mahsusi kwa ajili ya kufatilia usafirishaji wa nafaka katika Bahari Nyeusi.
(DPA, AFP, AP, Reuters)