Zelensky: Urefu wa vita unategemea msaada wa washirika
2 Oktoba 2023Zelensky ameelezea mfululizo wa hatua alizosema Umoja wa Ulaya unapaswa kuchukua ili kusaidia kumaliza vita nchini humo, ikiwa ni pamoja na kuongeza vikwazo vyake dhidi ya Urusi na Iran, ambayo imetoa ndege zisizo na rubani kwa vikosi vya Urusi.
Soma pia:Mawaziri wa mambo ya nje wa EU wakutana mjini Kyiv nchini Ukraine
Zelensky ameongeza kuwa ana imani kuwa Ukraine na ulimwengu mzima ulio huru unaweza kushinda katika mapambano haya. Ushindi wetu moja kwa moja unategemea ushirikiano wetu. Kadri tunavyochukuwa hatua thabiti kwa pamoja, ndipo vita hivi vitaisha kwa haraka na kwa haki, pamoja na kurejeshwa uadilifu kwenye eneo letu na dhamana ya kuaminika ya amani kwa Ulaya nzima.
Zelensky anataka mali ya Urusi iliyozuiwa kutumika kwa ujenzi mpya wa Ukraine
Kiongozi huyo pia amehimiza kuharakishwa kwa hatua kutoka kwa Umoja wa Ulaya kuelekeza mali za Urusi zilizozuiwa na kanda hiyo ili kwenda kufadhili ujenzi mpya wa Ukraine.
Borrell apendekeza msaada mpya kwa Ukraine
Wakati huo huo, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell, amemhakikishia Zelensky kwamba Umoja huo uko tayari kusimama na Ukraine kwa muda wote unaohitajika.
Soma pia: Ulaya yataka Marekani kufikiria upya msaada wake kwa Ukraine
Borrell amesema kwamba amependekeza msaada mpya wa pamoja wa Ulaya kwa ajili ya Ukraine wa thamani ya hadi dola bilioni 5.26 kwa mwaka ujao.
Baerbock asisitiza wito wake wa kinga kwa Ukraine
Huku hayo yakijiri waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesisistiza leo kuhusu wito wake wa kinga kwa Ukraine kabla ya msimu wa baridi ujao. Baerbock amesema hii itajumuisha kuongezeka wa ulinzi wa anga, usambazaji wa jenereta za umeme na uimarishaji wa usambazaji wa nishati kwa pamoja.
Urusi yakisia hali ya uchovu kwa mataifa ya Magharibi katika vita nchini Ukraine
Katika hatua nyingine, Urusi imesema inakisia kuongezeka kwa "hali ya uchovu" kwa upande wa mataifa ya Magharibi katika vita nchini Ukraine huku miito ikizidi kuongezeka miongoni mwa chama cha Republican cha Marekani ya kusimamishwa kwa msaada wa kiuchumi na kijeshi nchini Ukraine.
Soma pia:Zelenskiy asema hakuna chochote kitakachodhoofisha harakati zake za kuiangusha Urusi
Msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov, amesema leo kuwa kulingana na utabiri wao, upinzani utazidi kuongezeka katika mataifa mbali mbali kuhusu ufadhili nchini Ukraine na hili linaijumuisha Marekani.
Urusi yasema Marekani itaendelea kuhusika katika vita nchini Ukraine
Shirika la serikali ya TASS limemnukuu peskov akisema kuwa hali hiyo ya kuchoka itasababisha kusambaratika kwa uongozi wa kisiasa na kuongezeka kwa hali ya kutoelewana. Hata hivyo Peskov amesema anaamini kwamba Marekani itaendelea kujihusisha moja kwa moja na mzozo wa Ukraine licha ya mivutano inayogubika mazungumzo ya bajeti nchini Marekani na katika bunge la nchi hiyo juu ya msaada mpya wa kifedha kwa Ukraine.
Rais wa Marekani Joe Biden ameihakikishia Ukraine kutoipa mgongo wakati vita vya Urusi nchini humo vikiingia mwezi wake wa 20.