1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya katibu mkuu wa umoja wa mataifa Kofi Annan katika mashariki ya kati.

Omar Babu24 Agosti 2006

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan ataanza ziara yake ya mashariki ya kati hapo kesho ambapo atajaribu kuhimiza kuheshimiwa kwa mwafaka unaoregarega wa kusitishwa kwa vita kati ya Lebanon na Israil.

https://p.dw.com/p/CBIZ
Kikosi cha jeshi la India katika jeshi la kulinda amani nchini Lebanon.
Kikosi cha jeshi la India katika jeshi la kulinda amani nchini Lebanon.Picha: AP

Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umeanzisha shinikizo mpya kwa Israil kuondoa vikwazo vya safari za meli na ndege ilivyoviweka dhidi ya Lebanon.

Katika ziara hiyo, Annan anayetarajiwa pia kuzizuru nchi za Syria na Iran atasisitiza haja ya kutekelezwa kikamilifu azimio la Baraza la Umoja wa Mataifa lililosababisha kusitishwa kwa uhasama kati ya Israil na Hizbulla.

Maafisa wa umoja wa Mataifa hawajazungumzia mada zitakazoshughulikiwa katika ziara hiyo ya Annan lakini maafisa wa kibalozi wanasema Annan anatarajiwa kuwahimiza watawala wa Iran kulidhibiti kundi la Hizbulla kwa kuwa Iran ndio mfadhili mkuu wa kundi hilo la wanamgambo.

Aidha anatarajiwa kuiomba Syria kukoma kujiingiza katika maswala ya ndani ya Libnaan na kuhakikisha kwamba nchi hiyo haitumiwi kama mapitio ya silaha kwenda kwa makundi ya wanamgambo nchini Libnaan.

Annan anaainzia ziara yake mjini Brussels atakakohudhuria mkutano wa mawaziri wa mashauri ya kigeni wa mataifa ya Ulaya. Mkutano huo umeandaliwa kuratibu shughuli za kikosi kilichoongezwa cha Umoja wa mataifa kitakacholinda mpaka kati ya Libnaan na Israil.

Baadhi ya mataifa yangali na wasiwasi kuhusu majukumu ya kikosi hicho ambacho kuweko kwake kumeamuliwa na Umoja wa Mataifa.

Mchakato mzima wa uundwaji wa kikosi hicho ambacho ni muhimu kuhakikisha kuwekwa kwa amani kati ya hizbulla na Israil, umejikokota.

Maswala nyeti hayashughulikiwa mathalan kuhusu uhusiano wa kikosi hicho na majeshi ya Libnaan na Israil na pia wanamgambo wa hizbulla.

Aidha kuna wasiwasi kwamba yamkini majeshi hayo ya kimataifa yakajipata katika hali ya kutatanika endapo vita vitaanza tena.

Kamanda ya jeshi la Umoja wa Mataifa nchini Lebnaan Allain Pellegrini jana ametahadharisha kuwa hali inaweza kulipuka katika mzozo huo wa lebnaan.

O-TON PELLEGRINI

Nasema kwamba hali bado haijatengemaa. Kuna hali ya taharuki. Kosa dogo laweza kutumiwa kama kisingizio cha kuanza tena mapigano.

Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umezidisha shinikizo kwa Israil kuondoa vikwazo iliovyoviwekea Libnaan.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarrich amesema Annan ataiomba Israil kuondoa marufuku waliowekea Libnaan ya usafiri wa meli pamoja na ndege.

Dujarich amesema vikwazo hivyo vinapaswa kuondolewa haraka iwezekanavyo ili kuijenga upya Libnaan.

Msemaji huyo hakusema endapo Annan atakwenda Iran kabla ya mwisho wa mwezi ambayo ndiyo tarehe ya mwisho iliyowekwa na umoja wa mataifa kwa Iran kukomesha shughuli ya kurutubisha madini ya Uranium.

Msemaji mmoja wa kibalozi kutoka Ulaya amesema kwamba Annan amekuwa kwa muda mrefu akitaka kwenda Iran kulijadili swala la nyuklia.