Ziara ya waziri wa ulinzi wa Marekani nchini Afghanistan
12 Februari 2019Tunaanza na ziara ya waziri wa ulinzi wa Marekani Patrick Shanahan nchini Afghanistan. Amejaribu kutuliza hofu zilizochomoza baada ya rais Donald Trump kusema atawaondowa wanajeshi wa Marekani kutoka Afghanistan. Gazeti la "Rheinpfalz" linashuku kama matamshi yake yamesaidia kuwaondolea watu wasi wasi. Gazeti linaandika: "Matsamshi aliyoyatoa waziri wa ulinzi wa Marekani Patrick Shinahan alipokuwa ziarani nchini Afghanistan yalilengwa kuwaondolea watu wasi wasi. Lakini kwa waliotega vyema sikio, basi Shanahan hakulifikia lengo lake. Hakuna amri iliyotolewa ya kupunguza idadi ya wanajeshi, amesema waziri huyo. Ukosefu wa uwazi ni tatiizo na sio tu kwa serikali ya Afghanistan inayohofia wasije wakashindwa nguvu na wataliban pindi wanajeshi wa kigeni wakiondolewa. Ni tatizo pia kwa washirika wa serikali ya mjini Washington na hasa Ujerumani. Jeshi la shirikisho Bundeswehr linasaidia kwa kuwapatia mafunzo wanajeshi wasiopungua 1300 wa Afghanistan. Na msaada huo umewezekana kwasababu wanajeshi wa Marekani wanaadhamini usalama wao. Ikiwa wanajeshi wengi wa Marekani watahamishwa basi na wale wa Ujerumani pia hawatoweza kubakia."
Steinmeier akamilisha miaka miwili madarakani
Miaka miwili imekamilika tangu Frank-Walter Steinmeier alipochaguliwa kuwa rais wa shirkisho la jamhuri ya Ujerumani. Gazeti la "Frankenpost" linachambua: "Rais wa shirikisho anaendesha shughuli kimya kimya. Mara nyingi hakuna anaemsikia. Lakini ikilazimika basi rais huyu wa shirikisho hachelei kuwa mkakamavu. Kama ilivyoshuhudiwa baada ya uchaguzi mkuu uliopita, alipowashinikiza wana Social Democrat waliokuwa wakisita sita, waridhie serikali nyengne ya muungano wa vyama vikuu iundwe . Steinmeier anadhihirika kuwa rais anaefaa wa shirikisho katika kipindi hiki cha mitihani. Hawasumbui watu kwa hotuba za maadili kama alivyokuwa akifanya mtangulizi wake Joachim Gauck , badala yake anatumia sifa yake ya kuwa mtu mpole kuwafanya watu wajisikie wako salama."
Kongamano la chama cha CDU
Mada ya mwisho magazetini inahusu kongamano la chama cha kihafidhina cha CDU kuhusu sera ya wahamiaji na wakimbizi. Gazeti la Mittelbayerische Zeitung linaandika: "Kivuli cha "Tunaweza" bado kipo. Na chini ya kivuli hicgho kuna hisia za woga kukiri maamuzi mabaya yaliyopita na kwa namna hiyo pengine kuzidi kunyunyizia mafuta katika cheche za moto za wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia. Woga ni mkubwa pia kushadidia maamuzi yaliyopitishwa zamani na kwa namna hiyo kuzidi kupalilia pengine mfarakano chamani. Kwa namna hiyo kongamano la chama cha CDU haliwezi kutajwa kuwa ni fursa ya kujikomboa kama baadhi walivyokuwa wakitarajia."
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Yusuf Saumu