1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Westerwelle nchini Libya na mashariki ya kati

15 Juni 2011

Ziara ya waziri wa nje wa Ujerumani, Westerwelle, Afrika kaskazini na Mashariki ya kati, Uturuki baada ya ushindi wa tatu wa Erdogan? Na Ugiriki ndizo mada kuu magazetini.

https://p.dw.com/p/11aYy
Waziri wa nje wa Ujerumani Westerwelle (kushoto) akiamkiana na waziri mkuu wa Israel NetanyahuPicha: picture-alliance/dpa

Tuanzie lakini na ziara ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa ujerumani, Guido Westerwelle. Gazeti la "Braunschweiger Zeitung linaandika:

"Baada ya Libya, alielekea Israel- waziri wa mambo ya nchi za nje, Guido Westerwelle, anajitahidi kusaka amani. Na anaonyesha hasa mwanasiasa huyo ambae wiki chache zilizopita alizongwa na kishindo alipokuwa bado mwenyekiti wa chama chake cha kiliberali, kwamba hivi sasa ameridhika na nafsi yake, na amepania kuendesha wadhifa wake vyema zaidi. Lakini hata waziri wa mambo ya nchi za nje wa zamani, Joschka Fischer wa chama cha walinzi wa mazingira, amepita huko huko. Yaonyesha kila mtu anakwama huko. Westerwelle anajitahidi kwa upande wake kupatanisha. Wenye uwezo wa kuzuwia hali isizidi kuharibika ni wao wenyewe: Waisrael na Wapalastina- ingawa hali inayojitokeza ni nyengine kabisa.

Gazeti la Badische Neueste Nachrichten linaandika:

Tatizo la ziara hii ni kwamba Ujerumani haina usemi si Libya si Mashariki ya kati, na wala si kaskazini mashariki ya Afrika, seuze kuweza kushawishi hali ya mambo katika eneo hilo. Ziara ya Westerwelle kusema kweli mtu anaweza kuilinganisha na ziara ya mtu "asiyekuwa na nguvu."

Generalstreik in Griechenland am 15.06.2011
Wananchi wanagoma nchini UgirikiPicha: dapd

Mgogoro wa kiuchumi unaoitikisa Ugiriki umechambuliwa pia na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.Gazeti la "Nordwest-Zeitung" la mjini Oldenburg linaandika:

"Haikubaliki hata kidogo kwamba walipa kodi tu ndio waiokoe Ugiriki- kwa kutakiwa kuchangia viwango vikubwa vikubwa vya fedha. Wateja wa kibinafsi wanakwepa kabisa. Jambo hili halikubaliki. Mwishoe ufumbuzi rahisi utajitokeza, kama waziri wa fedha, Wolfgang Schäuble, anavyohoji. Muda wa mkopo utarefushwa na viwango vya riba kuzidishwa. Jambo hilo linaweza kuendelea kwa muda na kukubalika pia na wote wanaohusika. Lakini kama kwa namna hiyo Ugiriki itakuwa imesalimika, ni suala la kusubiri na kuona.

Türkei Wahlsieg AKP
Wafuasi wa chama tawala cha AKP wakipepea bendera ya UturukiPicha: dapd

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusiana na matokeo ya uchaguzi wa bunge nchini Uturuki. Gazeti la "Münchner Merkur" linaandika:

"Eti mhula watatu wa waziri mkuu aliyechaguliwa tena, Edogan, utasaidia kubainisha kiongozi huyo wa chama cha AKP anapanga kuielekeza wapi nchi hiyo? Baada ya kujipatia wingi wa viti bungeni na kujikusanyia maarifa ya miaka minane madarakani, Erdogan ana nguvu za kutosha kisiasa kufunua karata zake. Kwa mfano, linapohusika suala la Ulaya. Ikiwa Erdogan amedhamiria kweli kuiona Uturuki ikijiunga na Umoja wa Ulaya, basi wakati ndio huu umeshawadia wa kukamilisha masharti yaliyowekwa: Kwa mfano kutia saini itifaki ya Ankara na kufungua anga na bandari za Uturuki kwaajili ya ndege na meli za Cyprus .

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Miraji Othman