1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimbabwe: Muwafaka baina ya Mugabe na Tsvangirai umepatikana

Schadomsky, Ludgar17 Septemba 2008

Muwaka wa Zimbabwe utatiwa saini jumatatu

https://p.dw.com/p/FH8a
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe(kushoto) akipeana mkono na kiongozi wa Chama cha upinzani cha MDC, Morgan TsvangiraiPicha: AP

Baada ya miezi ya mashauriano na malumbano makali, serekali na upande wa upinzani nchini Zimbabwe jana zilifikia muwafaka. Muwafaka huo uliopatikana kutokana na upatanishi wa Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini unataka Rais Robert Mugabe, aachie sehemu ya madaraka yake kwa kiongozi wa upinzani, Morgan Tsvangirai. Tsvangirai, inasemekana, ataiongoza serekali, na polisi kuwa chini ya mamlaka yake. Jeshi litakuwa chini ya madaraka ya Rais Mugabe ambaye pia atakiongoza chombo kipya kitakachoitwa Baraza la Dola. Mnamo miezi 18 ijayo inatakiwa iundwe katiba mpya.

Mpatanishi huyo wa mzozo wa Zimbabwe amezidi kuwaweka watu roho juu. Ni jumatatu ijayo, pale patakapofanyika sherehe za kutia saini mapatano hayo, ndipo yaliomo ndani ya mkataba huo yatatangazwa, hasa juu ya suala la kuundwa serekali ya Umoja wa Taifa. Mtu achukulie kwamba hadi wakati huo, bado kutakuweko mashauriano makali: mfano, kujibu masuala kama vile vyama gani viwe na nafasi ngapi za mawaziri katika serekali ya mpito, upande gani utachukuwa mamlaka ya kusimamia majeshi korofi ya usalama, nani atalisimamia jeshi na nani ataunda baraza la mawaziri. Duru za habari kutoka Harare zinasema kuundwa kwa Baraza la Dola kumesababisha kupatikana suluhisho.

Jambo la kuvutia pia ni kama Morgan Tsvangirai ataweza kufanikiwa katika takwa lake kwamba yeye, kama waziri mkuu-mtarajiwa, awe na madaraka ya kumteuwa na kumfukza kazi waziri. Jambo hilo hadi juzi lilikuwa kizingiti kikubwa katika kufikia mapatano.

Mwishoni, muhimu kwa mafanikio au kutofanikiwa serekali hiyo ya mpito, ni kama Mzee Mugabe atakubali kughilibiwa ili katiba irekebishwe, kama vile upinzani wa sasa ambao utakuwa mshirika serekalini, unavotaka. Hiyo itamaanisha kwamba mamlaka yake, kama rais, yatapunguwa.

Wakati Wa-Zimbabwe itawabidi bado wayangojee matokeo ya mwenendo huu wa kisiasa, washindi wawili wa mapatano haya wako wazi: wa mwanzo ni Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini. Ile siasa yake ya diplomasia ya kimya kimya, ambayo kila wakati ilikuwa inalaumiwa vikali, imetoa matunda. Ikiwa muwafaka huu utadumu, kama inavoahidiwa, basi mwanasiasa huyo wa kutoka Ras ya Matumaini Mema atakuwa ameshinda katika ule usemi wake kwamba matatizo ya kiafrika yapatiwe suluhisho la kiafrika. Sifa pia itaiendea Jumuiya ya Uchumi ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, SADC, na kwa sehemu ndogo Umoja wa Afrika, AU.

Hata hivyo, kwa urahisi, Robert Mugabe, aliye hodari wa mbinu, amepata njia ya kujikwamua, anarejea tena katikati ya jukwaa la kisiasa, licha ya kwamba alishindwa katika uchaguzi na licha ya kwamba watu walishaanza mapema kumtoa maanani, kisiasa. Robert Mugabe amekuwa akiwanunuwa au kuwafyeka kikatili wapinzani wake wa kisiasa. Jamii ya kimataifa nayo ilibakishwa ikingoja kuweza kupeleka misaada muhimu ya kiutu kwa nchi hiyo ambayo uchumi wake umezorota kabisa hadi pale Mugabe alipochomoza kuwa mshirika wa kuutunga muwafaka huu.

Hadi jumatatu ijayo roho zitakuwa bado juu kwa wachunguzi wa mambo ya Zimbabwe na Wa-Zimbabwe wenyewe. Lakini baada ya mwongo mzima wa machungu ya kisiasa na miezi mitatu ya mashauriano marefu, sio muhimu kama mtu atasubiri kwa siku chache zaidi. Muhimu ni kwamba muwafaka huo wa jana udumu. Tetesi kutoka Harare zinasema kuna wapinzani fulani ambao hawajaufurahia muwafaka wenyewe. Sio tu Mugabe, lakini pia Chama cha MDC cha Morgan Tsvingirai kina majukumu. Lazima kijikomboe na ile mila ya Kiafrika inayosikitisha ambapo upinzani mwanzo kabisa unajitangaza wenyewe na kwa nadra unaendeleza siasa za ujenzi wa nchi. Ni ishara nzuri kwamba kikundi cha MDC kilichoasi cha Arthur Mutambara kimeukubali uwafaka huu.

Zimbabwe mbele yake ina weekendi ilio na msisimko, na tutarajie kwamba, kisiasa na kiuchumi, mbele kuna mapambazuko.