1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimbabwe yaomba msaada wa fedha kutoka Afrika Kusini

Richard Madete23 Agosti 2005

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe hivi karibuni amehudhuria makongamano mbalimbali barani Afrika. Kwa hiyo alipata nafasi ya kuongelea mambo mengi, lakini cha kushangaza hakusema kitu juu ya matatizo ya kisiasa nchini mwake. Kwa mujibu wa maelezo ya Umoja wa Mataifa zaidi ya watu milioni 4 nchini Zimbwabwe wanategemea msaada wa chakula. Thamani ya fedha inazidi kushuka na Zimbabwe hivi sasa ni nchi pekee kusini mwa Afrika ambayo uchumi wake unadidimia badala ya kustawi. Hali hii imepelekea Zimbabwe kuomba msaada wa fedha kutoka nchi za nje.

https://p.dw.com/p/CHf9
Nyumba zilizobomolewa mjini Harare
Nyumba zilizobomolewa mjini HararePicha: AP

Zimbabwe imeanguka kisiasa na kiuchumi na iko karibu kuwa muflisi. Kwa mantiki hii imeamua kuomba mkopo wa fedha kutoka Afrika Kusini. Tangu wiki kadhaa wahusika wanajadiliana jinsi ya kutoa msaada huu. Wengine wanahoji, kuna umuhimu kweli wa kuisaidia Zimbabwe? Kama jibu ni ndiyo, kwa kiasi gani na kwa kanuni zipi?

Mpaka sasa bado kuna mambo mengi ambayo hawajayapatia ufumbuzi, lakini mazungumzo yanaendelea, alisema naibu wa waziri wa mambo ya kigeni wa Afrika Kusini, AZIZ PAHAD. „Waziri wetu wa fedha na serikali ya Zimbabwe zinajadiliana juu ya jambo hili muhimu. Ni wazi kwamba tumeiwekea Zimbabwe kigezo cha kufanya mageuzi ya kina kwenye sera zake za uchumi, ingawaje maelezo kamili hayajatolewa.

Kwa upande mwingine tunanuia pia kupunguza mvutano wa kisiasa nchini Zimbabwe, hata kabla ya kufikiwa kwa utawala wa mshikamano wa kitaifa. TUnafurahi kwamba, pande zote za kisiasa zinaafikiana na jambo hili.“

Hata hivyo serikali ya Afrika Kusini chini ya rais Thabo Mbeki inaonyesha wazi msimamo wake. Imeweka masharti ya msaada wa fedha kwa Zimbabwe. Kama rais Mugabe anataka kupewa msaada huu, basi awe tayari kuzitumia kwa kushirikiana na upinzani nchini. Zaidi ya hapo pesa zenyewe hazitatolewa moja kwa moja bali zitapitia kwenye shirika la fedha ulimwenguni, IMF.

Msimamo huu unaungwa mkono na vyama vingi vya kisiasa nchini Afrika Kusini. Wote wanakubaliana kwamba, huu siyo muda wa kufanya mijadala ya kisiasa, limesema hata kanisa Katoliki nchini humo. Kanisa hili tayari limetoa misaada mingi ya kiutu ambayo inasafirishwa kwa malori makubwa ya mizigo. Askofu mkuu wa Cape Town, Jjongonkulu Ndungane amenukuliwa akisema, „lengo lao ni kuwasaidia wananchi wa Zimbabwe, na nchi zote za jirani.“

Itakumbukuwa kuwa Zimbabwe inatuhumiwa kwa mambo mengi hivi sasa: kwa mfano kwa ubomoaji na usafishaji wa vijumba vya ovyo mjini Harare. Chama tawala cha Zimbabwe kinautetea uamuzi huo. Matokeo yake, buldoza zilibomoa makazi ya wananchi wengi. Kwa mujibu wa makadirio ya Umoja wa Mataifa, katika muda mfupi tu, zaidi ya watu 700,000 walipoteza makazi yao na zaidi ya watu milioni 2 wameathiriwa na zoezi hilo.

Shirika la kimataifa la kusaidia watoto UNICEF limesema hali ya watoto nchini Zimbabwe ni mbaya kupindukia. Zaidi ya watoto 220,000 waliathirika na zoezi la usafishaji na ubomoaji wa nyumba za uchochoroni. Kwa hiyo hawana pa kuishi, hawana maji ya kutosha ya kunywa wala chakula na hawawezi kwenda shuleni.

Lakini waziri wa masuala ya usalama Didimas Buthasa alisema zoezi hilo lilikuwa muhimu. „Kulikuwa na biashara nyingi za magendo nchini humu. Wasichana walikuwa wanasimama kandokando ya barabara usiku na kujiuza kwa wenye magari. Kwa mtazamo wetu jambo hili halikuwa sahihi. Kwenye mitaa hiyo pia watu walikuwa wanafanya biashara haramu hata wakati wa mchana. Hili nalo tuliona ni jambo baya na ni kosa.“

Maelfu ya wakazi wanaishi sasa kwenye kambi za wakimbizi. Lakini shirika la kutetea haki za binadamu, Amnesty International limetoa ripoti isemayo hata kambi hizo huenda zikabolewa na utawala wa Zimbabwe kwenye zoezi jingine litakaloanza wiki chache zijazo.