Zuckerberg aliomba radhi bunge la Marekani
11 Aprili 2018Mmiliki na mwendeshaji mkuu wa mtandao wa kijamii Facebook, Mark Zuckerberg, ameliomba radhi bunge la Marekani kutokana na kushindwa kulinda taarifa binafsi za mamilioni ya Wamarekani kupitia kampuni ya ushauri wa kisiasa ya Cambridge Analytica na pia nia ya Warusi ya kuvuruga uchaguzi wa Marekani.
Katika mahojiano na bunge yaliyodumu kwa masaa matano jana Jumanne, Zuckerberg mara kwa mara alisikika akiomba msamaha kutokana na makosa hayo ya Facebook na kuweka wazi kwamba kampuni yake ilikuwa ikishirikiana na mshauri maalumu Robert Mueller katika uchunguzi wa Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani na kuongeza kuwa ilikuwa ikifanya kila linalwezekana kubadilisha utendaji wake baada ya kashfa ya kampuni ya huduma za ushauri wa kisiasa ya Cambridge Analytica, iliyofanya kazi na kampeni za urais za Donald Trump.
Huku akionyesha kutoridhishwa na majibu hayo ya Zuckerberg, Seneta wa jimbo la Dakota Kusini kutoka chama cha Republican John Thune alisema kampuni ya Facebok ina historia ya kuomba msamaha kwa miaka 14, kutokana na kile alichoita “maamuzi mabovu” kuhusiana na usiri kwenye taarifa za watumiaji. “Inawezekanaje msamaha wa hii leo ukawa na tofauti, aling’aka seneta Thune.
Zuckerberg alikiri kufanya makosa kadhaa katika uendeshaji wa kampuni ya Facebook na kuahidi kwamba kampuni yake itafanya kila linalowezekana kuhakikisha hatua vifaa itakavyotengeneza vitatumika kwa njia nzuri na salama.
Mgongano huo kwa kiasi kikubwa umeibua mtizamo mbaya dhidi ya kampuni hiyo na hata thamani ya hisa zake kuporomoka, lakini Zuckerberg alionekana kufanikiwa kukabiliana na hali hiyo.
Kwa ujumla, siku yake ya kwanza ya kutoa ushahidi mbele ya baraza la seneti ilipita salama. Na leo itakuwa ni siku ya pili ambapo atakabiliwa na maswali kadhaa kutoka kwa wabunge.
Zuckerberg alionyesha ukomavu mkubwa wa kujibu maswali ya wabunge.
Vikwazo bado ni vikubwa vinavyomkabili mwanzilishi huyo wa mtandao wa kijamii maarufu zaidi duniani wa Facebook mwenye miaka 33, Zuckerberg pamoja na kampuni yake. Facebok katika kipindi cha hivi karibuni imekuwa ikiendesha shughuli zake huku ikikabiliwa na kashfa mbaya zaidi ya kushindwa kudhibiti siri za taarifa za watumiaji wake, kufuatia ufichuzi wa mwezi uliopita kwamba kampuni ya huduma za ushauri wa kisiasa ya Cambridge Analytica, iliyokuwa na mashirikiano na kampeni za rais Trump, ilitumia taarifa za takribani watumiaji milioni 87 wa Facebok kinyume cha sheria.
Zuckerberg amekuwa katika safari ya kuomba msamaha katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, na hatimaye jana alipotojkea mbele ya bunge la Marekani. Ingawa mwanzoni alionekana kuyumba, lakini aliendelea kupata ujasiri kadri muda ulivyosogea. Kuna nyakati alionyesha msimamo madhubuti, hasa kutokana na maswali ya maseneta waliokuwa na ghadhabu, ambayo ni pamoja na kumtaka kupumzika kwa sasa kufuatia kashfa hiyo.
Kwa sehemu kubwa, majibu yake ya moja kwa moja ambayo hata hivyo aliyatoa kwa umakini, yalipunguza maswali ya shari kutoka kwa wabunge. Katika nyakati ambazo zilionekana kuwa ngumu zaidi, Zuckerberg alisema timu yake itahakikisha inafuatilia madai yanayotolewa na wabunge hao.
Kuhusiana na uchunguzi wa serikali dhidi ya Urusi kuingilia uchaguzi, ambao umechukua nafasi kubwa katika miezi kadhaa, amesema hakuwahi kufanyiwa mahojiano na timu ya mshauri maalumu Mueller, lakini alisema anajua kuwa wanafanya kazi pamoja, ingawa hakuelezea zaidi, kwa kuangazia umuhimu kuhusu kanuni za usiri wa uchunguzi huo.
Kwenye ushahidi wake, Zuckerberg alikiri kwamba hawakuangazia kwa uzito mkubwa suala kuhusu wajibu wao, na hilo lilikuwa kosa lao kubwa. Alisema "lilikuwa ni kosa langu kubwa na ninaomba msamaha". Nilianzisha Facebook, ninaiendesha, na ninawajibika na chochote kinachotokea". Aligusia pia hatua zinazochukuliwa na kampuni hiyo za kuzuia wadukuzi kufikia taarifa binafsi za watumiaji.
Mwandishi: Lilian Mtono/APE.
Mhariri: Mohammed Khelef