Zuma anusurika tena kutimuliwa uongozini
12 Novemba 2016Chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance kiliwasilisha hoja bungeni kufuatia ufichuzi wa idara ya kupambana na rushwa nchini humo kuwa familia tajiri ya Gupta iliruhusiwa na Zuma kufanya uteuzi wa mawaziri. Wakati ulipoanza mjadala bungeni kuhusu hoja hiyo ya kutokuwa na imani na rais Zuma, upinzani ulitaka iamuliwe kupitia kura ya siri. Hata hivyo chama cha rais Zuma cha ANC kiliuzima kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wabunge. Upinzani ulipata kura 126 huku upande wa serikali ukiungwa mkono na wabunge 214. Matokeo hayo yaliughadhabisha upinzani, na kiongozi wa chama kikuu cha Upinzani cha Democratic Alliance Mmusi Maimane kusema wanasiasa wanaoendelea kumlinda rais Zuma siku moja watajutia walichokifanya “Kura dhidi ya hoja hii ni kura ya kuendeleza ulaji rushwa ,ni kura ya kukubali wizi, ni kura ya kuruhusu utumizi mbaya wa madaraka. Lazima tuiweke mbele Afrika Kusini.Hebu tuziweke kando tofauti zetu na kuwafikiria watu wa taifa hili kwanza.”
Hii ilikuwa ni mara ya tatu kufanyika kura ya kutokuwa na imani na utawala wa rais Zuma katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja. Uchunguzi uliofanywa na idara ya kupambana na rushwa nchini humo ulipendekeza kundwa jopo la majaji kuchunguza madai ya uhalifu katika serikali ya Zuma. Idara hiyo ilipata ushahidi kuwa familia ya Gupta iliyo na uhusiano mkubwa na rais Zuma,imekuwa na ushawishi mkubwa katika uteuzi wa nyadhifa mbalimbali serikalini . Inadaiwa hata watu wawili walipewa nyadhifa za uwaziri na familia ya Gupta. Hata hivyo upande wa serikali umeshikilia kuwa rais Zuma anafanya kila awezalo kukabiliana na rushwa na pia kuimarisha uchumi wa taifa.Waziri wa maji na usafi wa mazingira Nomvula Mkonyane alimtaka kutovunjwa moyo na harakati za upinzani. Kwa rais Zuma sisi kama African National Congress tunasema kamwe dunia haiwezi kutambua mambo mazuri unayoyafanya mara millioni, lakini itakukosoa kutokana na kosa moja unalofanya. Usivunjike moyo.Sisi kama ANC hatuwezi kudai hatuna kasoro,lakini ni kupitia juhudi zetu tutaendelea kuzingatia maadili na kanuni za chama pamoja na katiba,Hakuna hata mmoja anaweza kudhubutu kutukosoa kutona na hilo."
Rais Zuma ,ameendelea kupata ungwaji mkono mkubwa kutoka chama chake cha ANC ambacho kinadhibiti karibu thuluthi mbili ya idadi ya wabunge 400. Rais huyo amekanusha kuwepo ushawishi wowote wa familia tajiri ya Gupta serikali ambayo inamiliki makampuni mbalimbali katika sekta ya madini na hata vyombo vya habari. Familia hiyo ya kihindi pia imekanusha kuhusika katika kosa lolote.
Mwandishi Jane Nyingi/Afrika link/APE/AFPE
Mhariri:Yusuf Saumu