Zuma na Ramaphosa wazungumza ana kwa ana
7 Februari 2018Kiongozi wa chama tawala nchini Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesema kwamba anafanya mazungumzo ya moja kwa moja na rais Jacob Zuma kuhusiana na makabidhiano ya madaraka na masuala yanayohusiana na nafasi ya Zuma kama rais wa taifa hilo.
Zuma aliyeko madarakani tangu mwaka 2009 na kukabiliwa na madai ya ufisadi amekuwa katika nafasi dhaifu tangu makamu huyo wa rais Cyril Ramaphosa alipochukua nafasi yake kama rais wa chama cha African National Congress, ANC mwezi Disemba. Ramaphosa amezungumzia kuhusu makabidhiano ya madaraka tangu alipochukua madaraka kwenye chama hicho.
Kwenye taarifa, Ramaphosa amesema yeye na Zuma wanatarajia kufikia hatma ya majadiliano yao na kutoa taarifa kwa taifa, katika kile alichosema kuwa " siku zijazo", na kuongeza kuwa mchakato huo ulikuwa ni fursa ya kuhitimisha suala hilo bila ya kuleta mtafaruku ama mgawanyiko ndani ya nchi hiyo.
Zuma anakabiliwa na ongezeko la shinikizo la kumtaka ajiuzulu kabla ya kumalizika kwa muda wake kutokana na kuelemewa na kashfa za ufisadi.
Mazungumzo yanayohusisha viongozi wakuu wa chama cha ANC yamekuwa yakiendelea kwa siku kadhaa wakati ambapo raia nchini humo wakisubiri kwa hamu kuelezwa kuhusu uwezekano wa Zuma kung'oka madarakani.
ANC yakiri kuridhishwa na mazungumzo kati ya Zuma na Ramaphosa.
Ripoti za awali zinadai kwamba Zuma alikuwa akiendelea kushikilia msimamo wake wa kutotaka kuondoka, lakini baadae ANC kilisema mazungumzo kati yake na kiongozi huyo wa ANC, Ramaphosa yalikuwa yenye manufaa.
Ramaphosa kupitia taarifa hiyo alisema, "usiku wa jana, rais Zuma na mimi tulianza majadiliano ya ana kwa ana kuhusu makabidhiano ya madaraka na masuala yahusuyo nafasi yake kama rais wa taifa hili". Majadiliano hayo yalikuwa ya kujenga na yaliweka msingi wa kufikia makubaliano kwa haraka kuhusu suala hilo kwa kuzingatia maslahi ya taifa na watu wake".
Mkutano wa vingozi wa chombo cha juu wa cha ANC, uliahirishwa siku ya Jumanne, kwa kuwa mazungumzo hayo yalionyesha kupiga hatua. Aidha hotuba kuhusu hali ya taifa iliyopangwa kutolewa wiki hii nayo ilisogezwa mbele katika tarehe ambayo haikutajwa.
Kama makamu wa rais na kiongozi wa ANC, Ramaphosa anapewa nafasi kubwa ya kuwa mrithi wa Zuma, iwapo atakubali kuondoka kabla ya kumaliza muhula wake.
Kiranja mkuu wa ANC, Jackson Mthembu ameonekana kuridhika kuhusu majadiliano kati ya viongozi hao wawili.
Mthembu amesema kwamba huenda hakutakuwa na haja ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na rais bungeni, iliyopangwa kupigwa Februari 22.
Muungano wa upinzani umeonya kwamba Zuma anaomba kinga ya kutoshtakiwa kama sehemu ya makubaliano ya yeye kuondoka madarakani, kimeripoti chombo kimoja cha habari nchini humo.
Wanachama wengi ndani ya ANC wanataka kuona Ramaphosa akichukua nafasi ya Zuma, ambaye ameharibu sifa ya chama hicho.
Mwandishi: Lilian Mtono/dpa.
Mhariri: Iddi Ssessanga