Zuma wa Umoja wa Afrika yuko Zimbabwe
25 Julai 2013Akizungumza alipowasili jana katika uwanja wa ndege wa Harare, Bibi Nkosazana Dlamini-Zuma alisema anatumai kiongozi wa ujumbe wa waangalizi kutoka Umoja wa Afrika, Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo watafika Zimbabwe ikiwa wataruhusiwa. Obasanjo atakayeuongoza ujumbe huo wa watu 80, anatarajiwa kuwasili Zimbabwe hivi karibuni.
Mnamo mwaka 2002, Obasanjo alikuwa miongoni mwa viongozi waliohisi kwamba Rais Robert Mugabe na chama chake Zanu-PF hawakushinda uchaguzi kihalali, na tangu wakati huo kumekuweko na mivutano zaidi kuhusiana na uchaguzi na kumalizikia kwa vyombo vya dola kuwakandamiza wapinzani. Dlamini Zuma alisema, yuko nchini humo kujionea tu jinsi mambo yalivyo kabla ya siku yenyewe ya uchaguzi.
Maswali muhimu kuhusu uchaguzi mkuu
Lakini ziara ya mkuu huyo wa Umoja wa Afrika inafanyika kukiwa na maswali mengi juu ya uwezekano wa uchaguzi kuwa huru na wa haki na ikiwa Zimbabwe itaruhusu waangalizi wa kigeni.
Tayari Rais Robert Mugabe amewakatalia waangalizi kutoka nchi za magharibi akisema, kwa sababu ya vikwazo dhidi yake na maafisa wengine wapatao 100 wa Zanu-PF kwa sababu ya ukandamizaji na ukiukaji wa haki za binaadamu.
Katika uchaguzi huu wa sasa Mugabe amesema atawaalika tu wale waangalizi aliowaita "marafiki."
Uhusiano wa Mugabe na SADC
Uhusiano kati ya Mugabe na Jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika SADC pia si mzuri baada ya kiongozi huyo mkongwe kukataa ushauri wa kuchelewesha uchaguzi hadi kwanza yamefanyika marekebisho ya kisiasa, ili kuepusha mgogoro uliozuka katika uchaguzi uliopita 2008 , baada ya chama cha Democratic Change MDC cha Morgan Tsvangirai kushinda viti vingi bungeni na kuongoza katika duru ya kwanza ya Uchaguzi wa Rais.
Wafuasi wa Mugabe wakisaidiwa na vyombo vya usalama wakawaandama wapinzani na Tsvangirai akajitoa katika duru ya pili ,akisema usalama wa wafuasi na wanachama wake ni muhimu. Mugabe akashinda bila ya mpinzani
Mgogoro huo ukasuluhishwa kutokana na juhudi za SADC na kuundwa serikali ya Umoja wa kitaifa.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 89 anawania kurefusha kipindi chake cha utawala akigombea kwa mara ya saba na akiwa ameshatawala kwa miaka 33 sasa.
Mwandishi:Mohammed Abdul-Rahman/afp, dpa
Mhariri: Mohammed Khelef