1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiAfrika

Afrika kugeukia nishati ya nyuklia kuzalisha umeme?

23 Oktoba 2023

Kwa mujibu wa Shirika la Nishati ya Nyuklia la Umoja wa Mataifa, IAEA, ni takriban asilimia 20 ya idadi ya watu nchini Burkina Faso wanaopata huduma ya umeme ilhali unahitajika na ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi.

https://p.dw.com/p/4XutT
Sehemu ya kinu cha nyuklia Ukraine, Zaporizhzhia
Sehemu ya kinu cha nyuklia Ukraine, ZaporizhzhiaPicha: Mathias Bölinger/DW

Hivi karibuni, serikali ya kijeshi nchini Burkina Faso ilitia saini tamko la nia inayolenga kuongeza usambazaji wa umeme nchini humo.

Kama sehemu ya makubaliano hayo, Rosatom, kampuni ya Urusi inayomilikiwa na serikali, itakuwa na jukumu la kujenga kinu cha nyuklia.

Hatua hii inaweza kuongeza kwa kiasi kikubwa kiwango cha umeme wa Burkina Faso ndani ya miaka michache ijayo. Lakini wataalam wana mashaka kuhusu uwezekano wa mradi huo.

Kwa wakosoaji kama vile Adrien Poussou, waziri wa zamani wa maridhiano ya kitaifa  katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, ujenzi wa kinu cha nyuklia ni aina ya propaganda za Urusi.

Soma pia:Urusi kwenye hatua za mwisho kujiondowa Mkataba wa Nyuklia

Mchambuzi huyo wa masuala ya siasa ameiambia DW kwamba inashangaza kwamba bara la Afrika, ambalo lina jua, linaweza kuwa na matatizo ya nishati na umeme.

Poussou amesisistiza kuwa nishati ya jua inapaswa kuwa suluhisho na sio makubaliano ya kujenga kinu cha nyuklia.

Burkina Faso sio nchi pekee ya kiafrika inayojihusisha na nishati ya nyuklia kwa ushirikiano na washirika wa kigeni.

Rosatom pia inalenga kuisaidia Mali katika kutumia nishati ya nyuklia kwa matumizi ya kiraia.

Mataifa ya Afrika kuzingatia nyuklia kama suluhisho?

Maeneo mengine ya Afrika pia yanazingatia nishati ya nyuklia kama chaguo la utoaji wa kiwango cha chini cha gesi ya kaboni kwa ajili ya kuzalisha umeme, pamoja na vyanzo vya nishati vinavyoweza kutumika tena. 

Mnamo mwezi Machi mwaka huu, wizara ya nishati ya Uganda ilitangaza kwamba nishati ya nyuklia itatumika kuzalisha umeme zaidi nchini humo kufikia mwaka 2031.

Viongozi wa mataifa ya Afrika wakiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres,
Viongozi wa mataifa ya Afrika wakiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres,Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Matayarisho ya kutathmini eneo la ujenzi wa kinu hicho cha kwanza cha nyuklia yanaripotiwa kuendeleakatika wilaya ya Buyende Mashariki mwa Uganda .

Katika mkondo huo huo, Uganda imetia saini makubaliano na Shirika la Kitaifa la Nyuklia la China (CNNC) kujenga kwa pamoja mitambo miwili ya nyuklia umbali wa kilomita 120 Kaskazini Mashariki mwa Kampala.

Soma pia:Ulimwengu usifeli Iran kama ulivyofeli Korea Kaskazini, IAEA

Nchi jirani ya Kenya imeeleza nia yake ya kuanza kujenga kinu cha nyuklia katika mwaka wa 2027, kwa makadirio ya muda wa miaka 10 ya ujenzi.

Wilaya za Kilifi na Kwale, ambazo ziko karibu na mji wa bandari wa Mombasa, kwa sasa zinazingatiwa kama maeneo ya ujenzi wa kinu hicho.

Shirika la nyuklia la Kenya, NuPEA, limesema kuwa pindi kinu hicho cha kitakapokamilika, kitaweza kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya nishati nchini kwa kuzalisha takriban megawati 1000 za umeme.

X.N. Iraki, mchambuzi kutoka chuo kikuu cha Nairobi, ameielezea DW dukuduku yake. Iraki anasema inashangaza kwamba nishati ya nyuklia inaanza kuzingatiwa ijapokuwa kuna nishati nyingi nchini humo.

Kwasasa, nchi hiyo inapata asilimia 90 ya nishati yake kutoka kwa vyanzo vinavyoweza kutumika tena hasa nishati inayotokana na joto la ardhini, maji na upepo.

Afrika kusini yatazamwa kama mfano

Serikali ya Kenya imeweka lengo la kutimiza mahitaji yake yote ya nishati kupitia vyanzo vinavyoweza kutumika tena ifikapo mwaka wa 2030.

Wataalamu kama vile Iraki wanahisi kwamba kuongezeka kwa nishati ya nyuklia barani Afrika si kwa manufaa ya bara hilo.

Kulingana na mtaalamu huyo, wawekezaji wengi wanavutiwa na hitaji la soko jipya.

Afrika Kusini inaweza kutumika kama mfano. Kwasasa taifa hilo ni la pekee barani Afrika ambalo imefanikiwa kuanzisha na kuendesha kinu cha nyuklia. 

Soma pia:Iran: Marekani ioneshe nia kufufuliwa mkataba wa nyuklia

Kinu cha pekee kinachofanya kazi barani humo kiko katika eneo la Koeberg karibu na Cape Town, kilichoanza kufanya kazi mwaka 1984.

Kwa miaka mingi, nchi hiyo imekuwa ikitafakari kuhusu upanuzi wa nishati ya nyuklia.

Kwa sasa, sehemu kubwa ya umeme wake unazalishwa kutoka kwa mkaa wa mawe, ambao una athari mbaya kwa hali ya hewa.
 

Umeme wa maji waongezeka Afrika, lakini ni zipi changamoto?