1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Kusini yakataa vikwazo dhidi ya Urusi

Josephat Charo
27 Mei 2022

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alifanya ziara barani Afrika kujaribu kutafuta washirka kupata kuungwa mkono msimamo wa nchi za magharibi kuhusu mzozo wa Ukraine.

https://p.dw.com/p/4By1T
Südafrika Besuch des Bundeskanzlers Olaf Scholz
Picha: Phill Magakoe/AFP

Gazeti la Süddeutsche ambalo lilikuwa na kichwa ha habari kilichosema "Kukataliwa kwa Scholz: Afrika Kusini yaendelea kukataa vikwazo dhidi ya Urusi". Mhariri anasema neno vita halikutoka kinywani mwa rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa wakati alipofanya mazungumzo na kansela wa Ujerumani Olaf Schoz. Akiwa ziarani Afrika Kusini Scholz alijaribu kumshawishi Ramaphosa aondokane na msimamo wa kuiunga mkono Urusi japo kwa muda kwa sababu ya vita vya Ukraine.

Scholz anasema aliguswa na kauli za Ramaphosa lakini ni wazi hajashawishika. Ramaphosa alitumia neno mzozo badala ya vita, akisema mzozo huo unaweza kutanzuliwa kupitia mdahalo, mashauriano na ushirikiano. Katika ziara yake ya siku tatu Afrika, Scholz alilenga kusisitiza msimamo wa Ujerumani kuendelea kulisaidia bara hilo, lakini pia kutafuta washirika kwa msimamo mkali dhidi ya Urusi.

Südafrika Besuch des Bundeskanzlers Olaf Scholz
Cyril RamaphosaPicha: Phill Magakoe/AFP

Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilisema ziara ya Scholz Afrika ilikuwa hatari lakini yenye mafanikio. Mwandishi wa gazeti hilo akiwa mjini Tillia, Franca Wittenbrink, anasema kansela anataka kuimarisha ushirikiano na Niger. Ziara ya Scholz ilifanyika wakati muafaka kabisa. Ijumaa wiki iliyopita kabla ya ziara hiyo Ujerumani iliamua kufikisha mwisho ushiriki wa jeshi la Ujerumani katika kikosi cha tume maalumu ya Umoja wa Ulaya inayotoa mafunzo nchini Mali, EUTM, na badala yake kuelekeza nguvu zaidi katika nchi jirani ya Niger.

Siku tatu baadaye katika ziara yake ya kwanza ya kuwatembelea wanajeshi wa Ujerumani nje ya nchi, Olaf Scholz alikuwa anasimama mahala ambapo jeshi la Ujerumani, Bundesweher, linapania kuwekeza nguvu zaidi kwa vikosi vyake eneo la Sahel katika siku za usoni. Kambi ya tume ya Umoja wa Ulaya iko Tillia, Niger ambako wanajeshi kadhaa wa kupambana vitani wamekuwa wakivisaidia kuwapa mafunzo wanajeshi wa vikosi maalumu vya Niger katika vita dhidi ya ugaidi. Wanajeshi chini ya 200 wa Ujerumani walikuwa wakishiriki katika tume hiyo iliyopewa jina la "Operation Gazelle", lakini sasa kutokana na mabadiliko wamefikia kiasi 260.

Mamlaka ya ujumbe wa amani sio leseni ya kuua

Gazeti la der Freitag ambalo liliandika kuhusu ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA. Mwandishi wa gazeti hilo alisema mamlaka imara ya ujumbe huo si leseni ya kuua. Mzozo nchini Mali una viashiria vya vita lakini hauko chini ya sheria za kimataifa kuhusu vita. Ujumbe wa kulinda amani wa MINUSMA kwa sasa una jumla ya wanajeshi 13,300 na maafisa 19,000 wa polisi kutoka nchi 36. Kwa kuzingatia ukubwa kikosi hicho kinafanana na tume maalumu ya "Resolute Support" iliyochukua nafasi ya tume ya amani nchini Afghanistan ISAF iliyotumwa mwanzoni mwa 2015.

Ukubwa wa tume hiyo unakaribiana na ule wa Mali ukijumuisha wanajeshi kati ya 13,200 na 16,300 kutoka nchi 41, ikiwa na mamlaka imara ya jumuiya ya kujihami ya NATO. Kama inavyofahamika tume ya "Resolute Support" ilifikia awamu yake ya mwisho takriban mwaka mmoja uliopita, wakati mwingine kwa wanajeshi kuondolewa haraka haraka. Uwezekano ni mdogo kwamba tume ya MINUSMA itafanana na "Resolute Support" kwa wakati huu, lakini hata uwepo wake kijeshi, ambao umetangazwa kuwa tume ya kuimarisha usalama na Umoja wa Mataifa, haina raslimali muhimu zinazohitajika.

Tedros Adhanom Ghebreyesus, Generaldirektor der Weltgesundheitsorganisation
Tedros Adhanom GhebreyesusPicha: Andreas Arnold/dpa/picture alliance

Gebreyesus achaguliwa tena kuiongoza WHO

Gazeti la Handelsblatt aliliandika kuhusu kuchaguliwa tena kwa mkuu wa shirika la afya ulimwenguni, WHO, Tedros Adhanom Gebreyesus, kuendelea kuliongoza shirika hilo kwa awamu ya pili. Mhariri anasema awamu nyingine afisini kwa mkuu huyo wa WHO inachukuliwa kuwa salama. Huku Ujerumani ikimuunga mkono Gebreyesus, raia huyo wa Ethiopia alikabiliwa na upinzani kutoka nchi nyingine ikiwemo nchi yake, Ethiopia. Akizungumza kabla kuchaguliwa tena kuiongoza WHO Gebreyesus alisema kama mtu aliyehudumu kama mwanajeshi mtoto anafahamu fika wanachokipitia raia wa Ukraine na kuitaka Urusi ikomeshe vita.

"Homa ya nyani si ukimwi"

Ni kichwa cha habari kilichoandikwa na gazeti la Neuer Zürcher. Mwandishi wa gazeti hilo Stephanie Lahrtz alisema virusi vya homa ya nyani ni tofauti na Sars-CoV-2 na virusi vya HIV vinavyosababisha ugonjwa wa ukimwi kwa njia mbalimbali muhimu na kwa hivyo hakuna haja ya kuhofia kutokea janga la mlipuko wa ugonjwa huo. Aliendelea kuandika kwamba kufikia Jumatatu iliyopita visa zaidi ya 100 vya maambukizi vilikuwa vimethibitishwa na visa karibu 100 vilivyoshukiwa kuwa homa ya nyani vilikuwa vimeripotiwa katika nchi 14.

Wanasayansi kote ulimwenguni wameelezea wasiwasi wao katika mahojiano na hofu ya kutokea mlipuko barani Ulaya na Amerika Kaskazini. Wataalamu wanatarajia visa zaidi vya maambukizi kuripotiwa katika siku na wiki zijazo. Ingawa homa ya nyani imefahamika tangu 1958, na visa vimekuwa vikishuhudiwa barani Afrika ambako maambukizi yamekuwa yakitoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, hakujawahi kutokea mlipuko mkubwa nje ya bara hilo. Kwa mujibu wa wataalamu, kuna watu wengi zaidi walioathiriwa barani Ulaya na Amerika Kaskazini kuliko ilivyowahi kugunduliwa nje ya Afrika tangu 1970.

(Inlandspresse)