1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Algeria: Bouteflika ashinda mhula wa nne

19 Aprili 2014

Rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika ameshinda uchaguzi wa rais wa Alhamis, na hivyo kupata mhula wa nne. Ameshinda kwa asilimia 81.53, akimpiga kikumbo mpinzani wake wa karibu Ali Benflis aliyeambulia asilimia 12.18.

https://p.dw.com/p/1Bkxq
Rais Abdelaziz Bouteflika aliyeshinda mhula wa nne kuiongoza Algeria
Rais Abdelaziz Bouteflika aliyeshinda mhula wa nne kuiongoza AlgeriaPicha: Reuters

Matokeo hayo yametangazwa na waziri wa mambo ya ndani Tayeb Belaiz katika mkutano na waandishi wa habari. Ufaransa ambayo ni mkoloni wa zamani wa Algeria, pamoja na jirani wa nchi hiyo, Moroko, zimekuwa nchi za kwanza kumpongeza Bouteflika kwa ushindi huo.

Belaiz amesisitiza kwamba uchaguzi huo ulifanyika katika mazingira ya uwazi, na kuongeza kuwa watu wamefanya chaguo lao kwa uhuru. Hata hivyo, Benflis ambaye kwenye siku ya uchaguzi alilalamikia kile alichokiita 'kasoro kubwa' katika maeneo yote ya nchi, amekataa kuutambua ushindi wa Bouteflika.

Mpinzani huyo wa Bouteflika amesema kuyatambua matokeo ya uchaguzi wa Alhamis ni sawa na kuunga mkono wizi wa kura, huku akilaani kile alichokitaja kuwa 'ushirika kati ya wizi, fedha za kutiliwa shaka, na vyombo vya habari ambavyo vimenunuliwa'.

Ushindi wa Bouteflika ambaye alipiga kura akiwa katika kiti chenye magurudumu ulikuwa ukitarajiwa na wengi. Watu wanaomuunga mkono walimiminika katika mitaa ya mji mkuu, Algiers mara tu baada ya vituo vya kura kufungwa Alhamis, na magazeti ya Ijumaa yalitabiri ushindi wake hata kabla ya matokeo kutangazwa.

Uchaguzi huo umefanyika mwaka mmoja baada ya Bouteflika kukumbwa na ugonjwa wa kiharusi na kulazwa hospitalini kwa miezi mitatu. Udhaifu wa afya yake ulimzuia kufanya kampeni katika uchaguzi wa wiki hii.

Ali Benflis, Mpinzani wa karibu wa Bouteflika
Ali Benflis, Mpinzani wa karibu wa BouteflikaPicha: Reuters

Matatizo yakithiri, uchumi washuka

Kuchaguliwa tena kwa Bouteflika ambaye ameiongoza Algeria tangu mwaka 1999 kumewagadhabisha vijana ambao wanapendelea mabadiliko. Nchi hiyo ya Afrika ya Kaskazini yenye utajiri wa raslimali ya nishati inakabiliwa na ufisadi mkubwa, ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana na uhasama wa kikabila.

Bouteflika anayo kazi ngumu ya kutekeleza ahadi yake ya uchaguzi, ambayo ni kupanua demokrasia na kutoa nafasi kwa kila mwananchi kushiriki katika maendeleo ya nchi.

Wachambuzi wa masuala ya Algeria wametahadharisha juu ya kuyumba kwa utengamano nchini humo kutokana na matatizo ya kijamii, ambayo serikali imeshindwa kuyapatia ufumbuzi. Mchambuzi wa kisiasa Rachid Tlemcani amesema kuchaguliwa tena kwa Bouteflika kutayazidisha matatizo hayo.

Licha ya wito wa Bouteflika kwa wananchi kuitikia kwa wingi zoezi la upigaji kura, ni asilimia 51.7 tu ya watu wenye haki ya kupiga kura nchini humo ambao walijitokeza, hiyo ikiwa idadi ndogo kabisa katika kipindi cha mika 20 iliyopita. Uitikiaji ulikuwa mdogo zaidi katika jimbo la Kabylie, ambako asilimia 25 tu ya wapiga kura walijitokeza.

Utengamano wenye gharama kubwa

Uamuzi wa Abdelaziz Bouteflika kugombea tena urais, ambo ulitangazwa mwezi February ulipokelewa kwa dhihaka kubwa na wakati mwingine ukosoaji mkali katika vyombo huru vya habari.

Vijana wengi hawakupendezwa na hatua ya Bouteflika kugombea tena
Vijana wengi hawakupendezwa na hatua ya Bouteflika kugombea tenaPicha: FAROUK BATICHE/AFP/Getty Images

Hata hivyo bado kiongozi huyo mkongwe ni kipenzi cha wengi, kutokana na mchango wake katika kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka ya 1990, ambavyo viliangamiza maisha ya watu wapatao 200,000. Katika uhariri wake wa Ijumaa, gazeti la Ach-Chouroq lilisema waalgeria wamechagua usalama na utengamano.

Kwa upande mwingine laki, gazeti la El Watan lililalamikia ''Usaliti ulioenezwa kwa hofu'' na kusema uchaguzi huo utakumbukwa kama tukio la kipuuzi.

Afisa mkuu wa Ikulu ya rais Amed Ouyahia amesema kupinga matokeo ya uchaguzi huo kunaweza kuifungua ''milango ya Jehanamu''.

Katika kile kinachotazamwa kama kitendo cha nadra cha kudhihirisha hasira ya umma dhidi ya utawala wa kiimla, kundi la vijana la ''Barakat' au 'Imetosha' lilundwa miezi miwili kabla ya uchaguzi kupinga kuchaguliwa tena kwa Bouteflika.

Hata hivyo maandamano ya hapa na pale ya vijana hao yalizimwa haraka. Barakat ilikuwa imeungana na vyama vitano vya upinzani kuwataka watu waususie uchaguzi wa Alhamis.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/RTRE

Mhariri: Iddi Ssessanga