Amani ya Syria iko mguu njiani mguu majanini
13 Aprili 2012Inatajwa kuwa ni amani ya wasiwasi, lakini angalau kuna ukimya ambao haujawahi kushuhudiwa kwa muda mrefu sasa. Ndani ya kipindi kinachozidi masaa 24, kutoka saa 12 asubuhi ya jana hadi sasa, majeshi ya serikali na yale ya upinzani yanaripotiwa kujizuia na mapigano ya moja kwa moja.
Akiliarifu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya maendeleo ya Syria, Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Kofi Annan, amesema ametiwa moyo na taarifa kwamba hali ya Syria imetulia, lakini akaonya kwamba bado utekelezwaji kamili wa wale wa amani haujafanyika.
Licha ya kusifu shwari iliyojitokeza kuanzia jana, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ametilia shaka uendelevu wake
"Hali ni shwari zaidi sasa. Tunaifuatilia kwa ukaribu sana. Dunia nzima inaiangalia, lakini kwa shaka, maana ahadi nyingi zilizowekwa na serikali huko nyuma haikuzitekeleza." Amesema Ban Ki-moon.
Kiongozi mwengine aliyeonesha kuitilia shaka dhamira ya serikali ya Syria, ni Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa, ambaye amesema hivi leo kwamba hauamini utiifu wa Rais Assad. Sarkozy ambaye pamoja na Rais Barack Obama jana waliitaka Syria kutekeleza kikamilifu mpango wa amani wa Annan, amesema lazima jumuiya ya kimataifa itekeleze wajibu wake, na sio kumtegemea Rais Assad.
Mapigano ya leo
Asubuhi ya leo, mapigano makali yameripotiwa katika mji wa Khirbet al-Joz kwenye jimbo la Idlib baina ya wanajeshi wa serikali na waasi. Haya ni baada ya yale ya jana, ambapo waasi waliokuwa wakilinda maandamano, waliwaua wanajeshi wawili wa serikali waliojaribu kuyasambaratisha maandamano hayo katika kijiji cha Bardeej kwenye jimbo la Hama.
Bado vikosi vya serikali vimeendelea kuonekana katika mitaa kadhaa ya Syria, ikiwa ni kinyume na kipengele muhimu kwenye mpango wa amani wa Kofi Annan.
"Jeshi bado halijajiondoa mitaani. Barabara zote zinadhibitiwa na wanajeshi, kuna vizuizi na watunguaji kwenye mapaa ya majumba. Lazima tusubiri na tuone ikiwa serikali inatekeleza kweli mpango wa amani. Wengi waliokwenda mitaani kuandamana ni kwa lengo la kubadilisha utawala." Amesema mwanaharakati mmoja aliye kwenye jimbo la Homs.
Jijini New York, Baraza la Usalama linatarajiwa hivi leo kulikubali ombi la Kofi Annan kupeleka timu ya wajumbe 30 nchini Syria kuangalia usitishwaji mapigano. Wajumbe 15 wa Baraza hilo walifanya mkutano wa ndani hapo jana kupitia rasimu ya azimio hilo, na kuna uwezekano mkubwa wa kulipitisha hivi leo.
Maandamano makubwa Syria
Nchini Syria kwenyewe kunatarajiwa kufanyika maandamano makubwa nchini kote, kikiwa kipimo kwa utawala wa Rais Bashar al-Assad, ikiwa kweli umeacha kuwashambulia waandamanaji. Upinzani umeitisha maandamano hayo, huku ukiwa na wasiwasi kwamba yatashambuliwa na wanajeshi wa serikali.
Mjini Washington, mawaziri wa nje wa mataifa makubwa kiviwanda duniani pamoja na Urusi, G8, wameukaribisha usitishwaji wa mapigano ulioanza nchini Syria, na kutaka Baraza la Usalama kuchukuwa hatua za haraka kufuatilia utekelezwaji wa mpango wa amani wenye vipengele sita wa Kofi Annan.
Hali ya amani ya wasiwasi iliyopo sasa inatajwa kuwa mafanikio kwa kazi ya wiki mbili mfululizo ya mjumbe wa kimataifa, Kofi Annan. Katibu Mkuu huyo wa zamani wa Umoja wa Mataifa amekitumia kipindi hiki sio tu kuzungumza na pande zinazopingana ndani ya Syria, bali pia mataifa yanayouunga mkono utawala wa Assad, zikiwemo China, Urusi na Iran, hatua ambayo wengi wanaitazama kama muhimu sana katika kuupatia suluhisho mzozo uliodumu miezi 13 sasa.
Pamoja na kusitishwa kwa mapigano, mpango wa amani wa Annan unataka kuachiliwa kwa wafungwa wote wa kisiasa, kuruhusiwa kwa mashirika ya misaada kufanya kazi zake na kufanyika kwa mazungumzo ya serikali na upinzani kuandaa kipindi cha mageuzi ya kisiasa nchini humo.
Mwandishi: Ulrich Leidholdt/DW/AFP/Reuters
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Daniel Gakuba