Annan: Assad aukubali mpango wa amani
27 Machi 2012Akiwa katika mji mkuu wa China, Beijing, alikokwenda kutafuta uungwaji mkono wa nchi hiyo, Annan ameiita hatua ya serikali ya Assad kukubali mpango wa amani wenye vipengele sita kama "dalili nzuri." Annan amesema kwamba hakuna namna ambapo mgogoro wa Syria utaachiwa uendelee na kwamba serikali ya Syria imefungua njia ya kupita kuelekea amani.
"Mgogoro hauwezi kuruhusiwa kuendelea bila kikomo. Na kama nilivyokwisha kuziambia pande zinazohusika, hawawezi kuzuia upepo wa mageuzi unaovuma. Wanapaswa kukubali kwamba mageuzi yamewadia." Amesema Annan.
Msemaji wa Annan, Ahmed Fawzi, amewaambia waandishi wa habari kuwa mjumbe huyo maalum wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, amesisitiza msimamo wake kwamba utekelezaji wa mpango huo wa amani utakuwa ufunguo sio tu kwa watu wa Syria, waliokwama kwenye mapambano, bali pia kwa eneo zima la Mashariki ya Kati na jumuiya ya kimataifa.
Mpango huo wa amani unataka kumalizwa kwa mwaka mzima wa vurugu kwa usitishwaji wa mapigano unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa, fursa kamili kwa mashirika ya kibinaadamu kufanya kazi zao, kuwachiwa watu wote waliokamatwa wakati wa machafuko na kuanzishwa kwa mchakato utakaopelekea mfumo wa vyama vingi ya siasa nchini Syria.
Waziri Mkuu wa China, Wen Jiabhao, amemuambia Annan kwamba nchi yake inaziunga mkono jitihada za mjumbe huyo juu ya Syria.
Mapigano na mauaji yaendelea
Lakini wakati Annan akipokea uthitisho wa Rais Assad juu ya utatuzi wa mgogoro, ndani ya Syria mabadiliko yoyote. Shirika la habari la Ujerumani, DPA, limeripoti kutokea kwa mapigano katika maeneo kadhaa hivi leo, ambapo watu 16 wameripotiwa kuuawa, sita kati yao wakiwa wanajeshi. Mapigano yameripotiwa katika maeneo ya kaskazini, kati na magharibi ya nchi hiyo.
Katika mpaka wa Syria na Lebanon, vikosi vya serikali vimepambana na waasi hadi ndani ya ardhi ya Lebanon. Mwanaharakati mmoja ameiambia DPA kuwa mapigano hayo yaliyodumu kwa dakika 20, yalianza kwanza ndani ya Syria, lakini vikosi vya serikali vikawafukuza waasi hadi kwenye eneo la al-Qaa, ambalo ni sehemu ya Lebanon.
Waasi hao ni wanachama wa Free Syrian Army, ambalo ni kundi la wanajeshi walioasi na kujiunga na upinzani tangu maandamano dhidi ya Assad yaanze mwaka mmoja uliopita. Shirika la habari la Syria, SANA, limesema Rais Assad ameutembelea mji wa Bab Amr kwenye jimbo la Homs, ambako ni kitovu cha upinzani dhidi ya serikali yake.
Marafiki wa Syria kukutana Istanbul
Na katika hatua nyengine, kundi linalojiita "Marafiki wa Watu wa Syria" linakutana Jumapili ijayo mjini Istanbul, Uturuki. Wizara ya Mambo ya Kigeni ya China imesema kwamba imealikwa kuhudhuria mkutano huo, lakini haitohudhuria.
Mkutano huo wa Istanbul unakuja katika wakati ambao Uturuki ikielekea kukubaliana na wazo la kuwepo eneo lisiloruhusiwa ndege kuruka ndani ya Syria, ili kulinda mipaka yake na pia raia wanaokimbia mapigano.
Mwanzoni Uturuki ilikuwa ikipangana na hatua hiyo, lakini wimbi la uasi unaondelea sasa nchini Syria, unaweza sana kuilazimisha serikali ya Tayyip Erdogan kuomba uungaji mkono wa kimataifa kuanzisha eneo hilo.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman