Ashton ahimiza ujumuisho
30 Julai 2013Mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton amesema katika ziara yake ya pili nchini Misri leo kuwa amekutana na rais aliyeondolewa madarakani Mohammed Mursi na kwamba hali yake ni nzuri na anauwezo wa kupata habari.
Umoja wa Ulaya utaendelea na juhudi zake za upatanishi ili kumaliza mzozo wa Misri. Hayo yamesemwa na mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton leo wakati akimaliza ziara yake mjini Cairo.
Akizungumza pamoja na makamu wa rais wa mpito Mohammed ElBaradei, Ashton amesema kuwa wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya watafika nchini Misri kuendeleza juhudi hizo. "Nitarejea, amesema Ashton , na kuongeza kuwa ni jukumu la wanasiasa wa Misri kufanya maamuzi sahihi."
Azungumza na Mursi
Ashton alikuwa na mazungumzo ya saa mbili na Mohammed Mursi alfajiri ya leo , huku duru zikilifahamisha shirika la habari la AFP kuwa aliondoka mjini Cairo kwa helikopta ya jeshi. Alikataa kusema ni wapi Mursi anakoshikiliwa ama kuelezea maelezo aliyoyatoa kwake.
Alikuwa mtu wa kwanza rasmi kuruhusiwa kukutana na Mursi tangu kuondolewa madarakani hapo Julai 3 na jeshi.
Ashton alikuwa akienda huku na huko kati ya makundi mbali mbali akisisitiza ujumbe wake kwa ajili ya amani, kuyajumuisha makundi yote yanayohusika katika mzozo huo katika utawala wa kiraia wa mpito katika taifa hilo la Kiarabu lenye wakaazi wengi.
Ni jukumu muhimu kwasababu kila kundi liko tayari kuzungumza nasi , sio kwasababu ya mbinyo wa nchi moja ama nyingine, ni kwasababu tunaweza kutekeleza jukumu hilo.
Msemaji wa ofisi ya mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Michael Mann amesema kuwa Ashton amekuwa akiwasiliana na pande nyingine zenye maslahi katika mzozo huo na amezungumza mara kadha na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry.
Alipoulizwa iwapo Umoja wa Ulaya unatumia mbinu gani kuibana Misri , Mann amesema Umoja wa Ulaya ni mtoaji mkubwa wa misaada kwa Misri, ambapo kiasi cha euro milioni 450 kilitolewa mwaka 2011 hadi 2013 kwa masharti maalum.
Hii haina maana kuwa kuna mbinyo, lakini katika miezi ya hivi karibuni hatujatoa msaada mkubwa kutokana na kukosekana maendeleo ya kisiasa, Mann amesema.
Mursi hatakuwamo katika mchakato mpya wa siasa
Akizungumza pamoja na Ashton katika mkutano mwingine na waandishi habari, makamu wa rais wa mpito anayehusika na masuala ya kimataifa Mohammed ElBaradei amesisitiza kuwa Mursi hatakuwa sehemu ya hatua za kisiasa zinazoendelea.
ElBaradei amesema kuwa kiongozi huyo aliyeondolewa madarakani hatakuwa na jukumu katika hatua za kisiasa za hapo baadaye, licha ya kuwatolea wito kundi la Udugu wa Kiislamu kushiriki.
Mursi ameshindwa lakini Udugu wa Kiislamu unaendelea kuwa sehemu ya hatua za kisiasa na tungependa washiriki katika hatua za kisiasa, amesema ElBaradei.
Ameieleza Misri kuwa inaingia katika "enzi mpya", baada ya maandamano ya Juni 30 ambayo yalisababisha kuondolewa madarakani kwa Mursi Julai 3.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe
Mhariri : Mohammed Abdul Rahman