AU, EU, Marekani zasikitishwa kutoachiliwa familia ya Bazoum
12 Agosti 2023Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell amesema wana taarifa kuwa Bazoum na familia yake wamekuwa wakinyimwa chakula, umeme, na huduma za afya kwa siku kadhaa sasa. Mkuu wa haki wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk, amesema hali anayozuiliwa Bazoum ni sawa na udhalilishaji wa ubinaadamu unaokwenda kinyume na sheria za kimataifa za haki za binaadamu. Kwenye tamko lake, Umoja wa Afrika umesema kutendewa vibaya kwa kiongozi aliyechaguliwa kidemokrasia hakukubaliki.
Soma zaidi: AU yazungumzia hali ya afya ya rais aliyepinduliwa Niger
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani, Annalena Baerbock, amesema wapangaji wa mapinduzi wanaweza kukabiliwa na hatua kali endapo jambo lolote baya litamtokea Bazoum na familia yake. Kauli kama hiyo imetolewa pia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken, ambaye amesema viongozi wa kijeshi wa Niger wamekataa kuiachilia familia ya Bazoum kama ishara ya nia njema. Bazoum, mkewe na mtoto wao wa kiume mwenye umri wa miaka 20, anayesemekana kuwa na matatizo ya moyo, wako mikononi mwa jeshi tangu tarehe 26 Julai, serikali yake ilipopinduliwa.