Rais Zelenskiy akutana na Macron, Scholz mjini Paris
9 Februari 2023Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz wamemhakikishia Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy kwamba nchi zao zitaiunga mkono Ukraine kadiri inavyohitajika. Ahadi hiyo ilitolewa wakati viongozi hao walipokutana Jumatano katika Ikulu ya Elysee mjini Paris.
Soma zaidi: Zelensky atumia ziara yake Uingereza kuomba silaha
Ufaransa "inadhamiria kuisaidia Ukraine kupata ushindi na kurejesha tena haki zake zote" alisema Macron kabla ya mlo wa jioni na Zelenskiy na Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani, na kuongeza kuwa Paris "itaendeleza juhudi" za kuisadia Ukraine kwa silaha.
Ukraine ni mwanafamilia wa Ulaya
Macron aliongeza kuwa Urusi haiwezi kuruhusiwa kushinda vita dhidi ya Ukraine na kwamba viongozi hao wawili, pamoja na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ambaye alisafiri kwenda Paris, watakuwa wakijadili mahitaji ya Kiev kuendeleza juhudi zake za vita.
Scholz pia alimhakikishia Zelenskiy kuendelea kwa msaada wa washirika. Kansela huyo wa Ujerumani alisema tangu uvamizi wa Urusi uanze karibu mwaka mmoja uliopita, Ujerumani na washirika wake wameiunga mkono Ukraine "kifedha, kwa misaada ya kibinadamu na kwa silaha."
Soma zaidi: Urusi yaongeza hujuma nchini Ukraine msimu huu wa baridi
"Tutaendelea kufanya hivyo kwa muda mrefu iwezekanavyo," Scholz aliwaambia waandishi wa habari.
Scholz alisema kuwa viongozi katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya siku ya Alhamisi watatuma ishara ya mshikamano thabiti na Ukraine. "Ninapeleka ujumbe ulio wazi mjini Brussels, kwamba mahali pa Ukraine ni katika familia ya Ulaya," alisema.
Baada ya kuahidiwa vifaru, Ukraine sasa yataka ndege na maroketi
Wakati huo huo, Zelenskiy alizitaka Ufaransa na Ujerumani kuongoza mabadiliko ya mtazamo kwa kuipa nchi yake ndege za kisasa za kivita. "Tuna muda mchache sana. Ninazungumza sasa kuhusu silaha zinazohitajika ili tuweze kusimamisha vita vilivyoanzishwa na Urusi dhidi yetu," alisema rais huyo wa Ukraine.
Soma zaidi: Guterres ahofia kuenea kwa vita vya Ukraine
"Ufaransa na Ujerumani zina uwezo wa kubadilisha mwelekeo na hayo nimeyaona katika mazungumzo yetu leo. Kadiri tunavyopata silaha nzito za masafa marefu na marubani wetu kupata ndege za kisasa ... ndivyo uchokozi huu wa Urusi utakavyohitimishwa," aliongeza Zelenskiy.
Kabla ya kwenda Brussels, mapema Jumatano Zelenskiy alitembelea London. Hii ni safari yake ya pili nje ya nchi yake tangu Urusi ilipovamia Ukraine Februari 24, 2022, baada ya ziara yake ya mwezi Disemba mjini Washington, ambapo alikutana na Rais Joe Biden na kulihutubia Bunge la Marekani. Baadaye leo Alhamisi, Zelenskiy ataungana na viongozi wa Umoja wa Ulaya katika mkutano wa kilele mjini Brussels.
Vyanzo: msh/jcg (AFP, AP, dpa, Reuters)