Baadhi ya nchi za NATO zimetofautiana kuhusu Libya
23 Juni 2011Wito wa kusitishwa mashambulizi yalitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Franco Fratini, wakati alipolihutubia Bunge la nchi hiyo kwamba hatua hiyo itakuwa ya msingi katika kufanikisha misaada ya haraka ya kiutu kuwafikia walengwa.
Fratini amesema pamoja na kufanikisha hilo, pia utakuwa mwanzo wa kuifanikisha suluhu ya kisiasa nchini Libya.
Hata hivyo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Italia alitolea ufafanuzi wa kauli hiyo kwa kusema mpaka sasa Italia haijaandaa mapendekezo yeyote, na kwamba inachohitaji ni mawazo yeyote yatakayosadia kupunguza maafa nchini humo.
Kutokana na kauli hiyo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa, Bernard Valero, amesema wanapaswa kuongeza kumbana Gaddafi kwa kuwa kuregeza kamba kunaweza kusababisha akajipanga upya na kujijengea uwezo.
Wazo hilo pia liliungwa mkono na Uingereza, kama nchi mshirika na Ufaransa, ambao walianza kwa pamoja katika kuitekeleza operesheni ya kuzuwia kuruka ndege juu ya anga ya Libya, kwa shabaha ya kuwanusuru raia wa Libya dhidi ya majeshi ya Gaddafi, ikiwa utekelezaji wa azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.
Msemaji wa Waziri Mkuu wa Uingerera, David Cameron, amesema uamuzi wa msingi kwa sasa ni kuengeza shinikizo dhidi ya Gaddafi. Amesema ametoa wito wa kusitisha mapigano mara kadhaa, lakini mpaka sasa hakuna hata mara moja ametekeleza jambo hilo.
Katika hatua nyingine jana jioni, Gaddafi aliituhumu NATO kwa kufanya mauaji dhdi ya raia wasio na hatia na kuahidi kulipa kisasi.
Akizungumza kupitia sauti iliyorekodiwa katika televisheni ya serikali ya nchi hiyo, Gaddafi alisema " siku moja tutawafanyia kama mnavyotufanyia na majumba yenu yatalengwa!".
Katika mazungumzo hayo, kiongozi huyo alirejea mashambulizi ya june 19 ambayo yamesababisha vifo vya watu 15 kwa kuita kitendo hicho kilichofanywa na NATO kwa ni cha kihalifu.
Gaddafi amesema haogopi kifo na kwamba atapigana hadi mwish. Akizungumza kwa sauti inayoashira kuwa na hasira, alisema "hakuna tena maafikiano baada ya kuwauwa watoto na wajukuu zetu."
Kauli ya Gaddafi inafuatie ile ya Katibu Mkuu wa NATO, Anders Forgh Rasmussen, kwamba umoja huo hautasitisha mashambulizi kwa kuwa kufanya hivyo kutasababisha vifo zaidi kwa raia wa Libya.
Waasi, kwa upande wao, wamesema hawatasita, wataendelea na mapigano dhidi ya utawala wa Gaddafi mpaka wafanikishe ukombozi wa nchi hiyo.
Mwandishi:Sudi Mnette RTR
Mhariri: Miraji Othman