1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Libya na Waasi wapo katika mazungumzo.

17 Juni 2011

Mjumbe wa Urusi nchini Libya, Mikhail Margelov, amesema serikali ya Libya ipo katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa maja kuhusu mgogoro wa nchi hiyo huku kukitolewa wito wa kufanyika kwa uchaguzi

https://p.dw.com/p/11d4j
Mapambano kati ya vikosi vya serikali na waasiPicha: picture alliance / dpa

Mwakilishi wa Rais Dmitry Medvedev nchini Libya, Michael Margelov, jana aliwasili mjini Tripoli kwa siku moja, ziara iliyofanyika baada ya ile alioifanya katika ngome ya waasi wa nchi hiyo, mjini Benghazi.

Baada ya kuzungumza na Waziri Mkuu wa Libya, Baghdadi al Mahmudi, Margelov alisema ana hakika kwamba kuna mazungumzo ya moja kwa moja ambayo yameanza na yanaendelea kati ya serikali ya Libya na Waasi.

Margelov, ambae amenukuliwa na Shirika la Habari nchini Urusi, ITAR-TASS, alisema Waziri Mkuu wa Libya amemueleza mazungumzo ya mwisho yamehitimishwa hivi karibuni mjini Paris, Ufaransa.

Hata hivyo, kwa mujibu wa mjumbe huyo wa Urusi, Waziri Mkuu huyo hakusema kilichojadiliwa katika mazungumzo hayo ambayo pia hayajathibitishwa na upande wa waasi.

Katika mazungumzo hayo, Mahamudi amesema suala la Gaddafi kuondoka madarakani ni la "mstari wa hatari" ambao hauwezi kuvukwa, pamoja na kuwepo kwa wito wa mataifa kumtaka aondoke.

Kauli kama hiyo waziri Mkuu huyo wa Libya aliitoa katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Tripoli, akisema dhamira yao kubwa ni mazungumzo yatakayowaunganisha Walibya.

Kauli ya Waziri Mkuu Mahamudi inafuatia ile ya mtoto wa Gaddafi, Seif al Islam, ambae anasema suluhisho pekee la mkwamo wa kisiasa nchini Libya ni kufanyika uchaguzi huru na wa haki katika miezi michache ijayo.

Kauli hiyo imepokewa kwa namna tofauti na Marekani ambayo imesema kwanza imechelewa na siku za kiongozi wa Libya kuwepo madarakani kwa hivi sasa zinahesabika.

Hillary Clinton
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary ClintonPicha: AP

Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton ameyatuhumu majeshi ya Gaddafi kwa kufanya ubakaji na unyanyasaji dhidi ya wanawake kama silaha ya kivita.

Hillary Clinton amesema Marekani imesikitishwa sana na ripoti ilionesha kwamba serikali katika maeneo ya Mashariki ya Kati na Afrika kaskazini zinatumia unyanyasaji wa kijinsia kuwaadhibi waandamanaji.

Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa Uhalifu wa Kivita, Luis Moreno Ocampo, wiki iliyopita alisema kuna ushahidi kwamba serikali ya Libya imenunua dawa za kuongeza nguvu za kiume(Viagra) na kuzigawa kwa vikosi vyake ili vifanikishe kazi ya ubakaji.

Mapambano yanendelea kwa namna tofoati nchini humo, jitihada za waasi kuelekea ngome ya serikali ya Libya mjini Tripoli zimekuwa zikisuasua huku ndege za kivita za NATO zikiendelea kuyashambulia makazi ya Gaddafi na maeneo mengine.

Hata hivyo juhudi zote hizo, zinaonekana kama zimeshindwa kuhitimisha utawala wa miongo minne wa kiongozi hiyo wa Libya.

Mwandishi: Sudi Mnette/Afp/Reuters

Mhariri: Miraji Othman