Ban Ki Moon amtaka Gadaffi asitishe mashambulio
7 Machi 2011Kwa mujibu wa afisi yake ya mawasiliano,uongozi wa Libya huenda ukalazimika kuwajibika endapo utazikiuka sheria za kimataifa.Ili kuiweka sawa Libya,Ban Ki Moon amemteua waziri wa mambo ya nje wa Jordan wa zamani,Abdelilah Al-Khatib kuwa mjumbe maalum atakayeushawishi uongozi wa Libya kukaa katika meza ya mazungumzo ya dharura.
Azma ya mazungumzo hayo ni kulitafutia suluhu tatizo la wakimbizi wanaoyakimbia machafuko nchini humo.
Pindi waziri wa mambo ya nje wa Libya alipoiridhia mipango hiyo,Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa una mpango wa kuipelekea kundi maalum la wataalam watakaoitathmini hali halisi na mahitaji yake.Wakati huohuo,kuna hofu kuwa Libya huenda ikaingia katika kipindi cha vita vya wenyewe kwa wenyewe.Mapigano makali yameripotiwa kutokea pale vikosi vinavyomuunga mkono Kanali Muammar Gaddafi vilipojaribu kuiteka nyara miji ya Misrata,Az-Zawiya na Ras Lanuf inayodhibitiwa na waasi kwa sasa.