Baraza la Haki la UN kumteua mchunguzi huru dhidi ya Urusi
7 Oktoba 2022Baraza hilo la Haki za binadamu lenye wanachama 47 limepasisha pendekezo hilo lililowasilishwa wiki iliyopita na nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya isipokuwa Hungary. Muda mfupi kabla ya kupiga kura hiyo huko mjini Geneva, Shirika la kutetea haki za binadamu la Russia Memorial lilitajwa kuwa mshindi mwenza wa Tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka huu wa 2022.
Pendekezo la awali lilidhihirisha wasiwasi kuhusu kufungwa kwa wingi kwa vyombo huru vya habari, mashirika yasiyo ya kiserikali na makundi ya upinzani nchini Urusi. Wanachama walio wengi wa Baraza hilo waliafiki kuteuliwa kwa "kamati maalum" itakayoendelea kufuatilia matukio ya ukiukaji wa haki nchini Urusi, kwa kutegemea kwa kiasi fulani msaada kutoka kwa makundi ya wanaharakati wa urusi ambao bado wapo nchini humo na hata nje ya nchi.
Soma zaidi:Umoja wa Mataifa kuamua juu ya uchunguzi Ukraine
Urusi ambayo ilikuwa mwanachama wa Baraza la Haki za binadamu hadi mapema mwaka huu kabla ya kujiondoa kwake, imechukua hatua kadhaa za kufifiza upinzani wa ndani kutokana na vita vyake nchini ukraine, ikiwa ni pamoja na kupitisha sheria inayopiga marufuku kueneza habari "za uongo" kuhusu jeshi la Urusi.
Soma zaidi: Urusi yasimamishwa uanachama baraza la haki za Binaadamu la UN
Idadi ya vifo Zaporizhzia yaongezeka
Idadi ya waliofariki kutokana na shambulio la makombora katika eneo la makazi huko Zaporizhzhia imeongezeka na kufikia watu 11 huku kwa mara ya kwanza kabisa, ndege zisizo na rubani na zilizobeba vilipuzi zimefanya mashambulizi katika mji huo wa kusini mwa Ukraine na ambako kuna kinu kikubwa zaidi cha nyuklia barani Ulaya. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amelaani mashambulizi hayo:
" Urusi imeshambulia tena kwa makombora. Kwa bahati mbaya, kuna vifo, watu waliojeruhiwa, na majengo yaliyoharibiwa. Huko Zaporizhzhia, baada ya shambulio la kwanza la roketi, wakati watu wakiondoa vifusi, Urusi ilifanya shambulio la pili la roketi. Ni uovu na ukatili wa hali ya juu. Kumekuwa na maelfu ya matukio kama haya. Na kwa bahati mbaya mengine zaidi huenda yakashuhudiwa."
Soma zaidi: Amnesty: Urusi imefanya uhalifu wa kivita, Ukraine
Mapigano karibu na Kiwanda cha Nyuklia cha Zaporizhzhia yamewatia wasiwasi wakuu wa Shirika la Kimataifa la Kudhibiti Nishati ya Atomiki - IAEAA, wanaofahamisha kuwa ajali katika kinu hicho inaweza kusababisha uvujaji kiasi mara 10 ya mionzi hatari ambayo ilishuhudiwa katika ajali mbaya zaidi ya nyuklia iliyotokea Chernobyl miaka 36 iliyopita.