Baraza la Usalama kuongeza waangalizi wake Syria
22 Aprili 2012Balozi wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa, Gerard Araud, amesema hati ya azimio hilo ambayo ilijadiliwa kwa saa kadhaa hapo jana, inawasilishwa katika kikao cha Baraza la Usalama kinachoktaa saa 5:00 asubuhi (kwa saa za Marekani) siku ya Jumamosi kwa ajili ya kupigiwa kura.
Naye balozi wa Urusi kwenye Umoja huo, Vitaly Churkin, alielezea matarajio yake kwamba azimio hilo litapigiwa kura bila ya kupingwa leo.
Lakini rais wa sasa Baraza la Usalama, balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Susane Rice, amesema kuna uwezekano wa kuwa si “mataifa yote 15 yatakayokubaliana na maneno yaliyomo kwenye azimio hilo na kwamba mengine yanaweza kuwa na maagizo kutoka kwa serikali zao.”
Rasimu ya mwisho ya azimio hilo ilizichanganya hati mbili zilizowasilishwa kwenye Baraza na Urusi na mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya, ambapo lina muafaka wa pande zote.
Ulaya yataka kauli kali zaidi, Urusi yapinga
Mataifa ya Ulaya yalitaka azimio hilo lijumuishe kitisho cha vikwazo visivyo vya kijeshi dhidi ya Syria ikiwa itashindwa kuondoa vikosi vyake na silaha nzito katika miji na mitaa, lakini China na Syria zinapinga vikwazo dhidi ya serikali ya Rais Bashar al-Assad na hatimaye kipengele hicho kiliondolewa.
Badala yake azimio hilo limetumia maneno yaliyo kwenye azimio la Jumamosi iliyopita lililoruhusu utumwaji wa timu ya awali ya waangalizi 30 wa Umoja wa Mataifa nchini Syria. Linaelezea dhamira ya Baraza la Usalama kutathmini utekelezwaji wa azimio hilo jipya na “kuzingatia hatua zaidi. Tafauti ya msingi katika maneno ya asili ni ikiwa kunalazimika kuwepo kwa masharti maalum ya upelekwaji wa kikosi hicho.
Ban alimlaumu Rais Bashar Assad kwa kushindwa kuheshimu mpango wa amani wenye vipengele sita wa mjumbe wa kimataifa, Kofi Annan, ulioanza kufanya kazi wiki moja iliyopita. Amesema ghasia zimeendelea na ametaka kuwepo na usimamishwaji w amara moja wa mashambulizi yote ya serikali na wapinzani.
Rasimu iliyowasilishwa mwanzoni na Umoja wa Ulaya ilisema kabla ya kutumwa kwa timu mpya ya waangalizi wapya, Katibu Mkuu ajiridhishe kwamba Syria imetekeleza ahadi yake ya kuondosha wanajeshi na vifaa vya kivita mitaani. Rasimu iliyowasilishwa na Urusi haikuwa na masharti yoyote yale.
Muafaka wa rasimu za Ulaya na Urusi
Lugha ya mapatano katika rasimu ya mwisho ya azimio hilo inasema uongezwaji wa timu ya waangalizi “lazima uendane na tathmini ya katibu mkuu juu ya maendeleo nchini Syria, likiwemo suala la usitishaji wa ghasia.
Balozi wa Ufaransa, Araud, alisema Baraza la Usalama linataka kutuma waangalizi wake haraka iwezekanavyo “lakini wakati huo huo lazima tutilie maanani hatari inayowakabili na hiyo ndiyo sababu katibu mkuu lazima atathmini hali ilivyo nchini Syria.”
“Ni aina mpya ya ujumbe,” Araud aliwaambia waandisi wa habari. “Ni mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kuwatuma waangalizi wake katika eneo la vita kwa sababu bado kuna mapigano…bado kuna ghasia.”
Balozi wa Urusi, Churkin, alisema kwamba anatarajia kuwa utumaji wa kikosi madhubuti cha waangalizi 300 wa Umoja wa Mataifa utatoa ishara nzuri na madhubuti ya kisiasa kwa serikali na upinzani nchini Syria.
“Tunatarajia watu ambao wamekuwa na ushujaa wa kutosha kuenda huko wajuwe kuwa hawako bure bure na kwamba Sekreterieti na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wabakuchukulia zoezi hili kwa umakini mkubwa,” alisema Churkin.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP
Mhariri: Stumai George