1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Usalama laidhinisha azimio la kusitisha vita Gaza

Sylvia Mwehozi
11 Juni 2024

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo jana liliidhinisha kwa wingi azimio lake la kwanza la kuunga mkono mpango wa kusitisha vita vya miezi minane kati ya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4gtmL
Marekani, New York | Umoja wa Mataifa
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Picha: Angela Weiss/AFP/Getty Images

Azimio hilo lililoandaliwa na Marekani, limeidhinisha pendekezo la kusitisha mapigano lililotangazwa na Rais Joe Biden, ambalo Washington inasema kuwa Israel imekubaliana nalo. Linatoa wito kwa kundi la wanamgambo la Hamaskukubaliana na awamu tatu za mpango huo. Azimio hilo ambalo lilipitishwa na wajumbe 14 kati ya 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kasoro Urusi tu ambayo ilijizuia, linazitaka Israel na Hamas "kutekeleza kikamilifu vipengele vyake bila ya kuchelewa na bila masharti".

Soma: Blinken asisitiza mpango wa baada ya vita wa Gaza

Linda Thomas-Greenfield, ni balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa na amesema kuwa; "Leo Baraza hili limetuma ujumbe wa wazi kwa Hamas! kubalini makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoko mezani. Israel tayari imekubali mpango huu na mapigano yanaweza kusitishwa leo ikiwa Hamas itafanya vivyo hivyo. Narudia: mapigano yanaweza kusimama leo."

Gaza -vita-kambi ya wakimbizi ya Nuseirat
Uharibifu wa makazi kambi ya wakimbizi wa NuseiratPicha: Jehad Alshrafi/AP Photo/picture alliance

Suala la iwapo Israel na Hamas zitakubaliana juu ya mpango huo bado ni kitendawili, lakini uungwaji mkono mkubwa wa azimio hilo katika chombo chenye nguvu zaidi cha Umoja wa Mataifa, kunazidisha shinikizo zaidi kwa pande zote mbili kuidhinisha pendekezo hilo.

Soma: Israel yaendelea kuipiga Gaza huku idadi ya Wapalestina waliouawa wakati wa kuwaokoa mateka ikifika 274

Kundi la Hamas tayari limesema kuwa linakubaliana na azimio hilo na liko tayari kwa majadiliano juu ya vipengele vilivyomo. Hayo yalielezwa na afisa mwandamizi wa Hamas Sami Abu Zuhri, alipozungumza na shirika la habari la Reuters mapema siku ya Jumanne, akiongeza kuwa ni wajibu wa Washington kuhakikisha kwamba Israel inaheshimu mpango huo. Miongoni mwa aliyoyataja afisa huyo kuhusu mpango huo ni kuondolewa kwa vikosi vya Israel na kubadilishana wafungwa wanaoshikiliwa na Israel.

"Utawala wa Marekani unakabiliwa na mtihani halisi wa kutekeleza ahadi zake katika kukomeshwa kwa uvamizi huo mara moja katika utekelezaji wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa."

Hayo yanajiri wakati waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken anaendelea na ziara yake kanda ya Mashariki ya Kati aliyoianza siku ya Jumatatu katika mwendelezo wa jitihada za kufikiwa makubaliano ya kusitisha vita.

Blinken akiwa  Israel
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alipokutana na waziri mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Amos Ben-Gershom/GPO/dpa/picture alliance

Blinken amekutana na rais wa Israel Isaac Herzog kama sehemu ya juhudi zinazoendelea za upatanishi zinazofanywa na Marekani, Qatar na Misri za usitishaji mapigano. Ziara ya Blinken kanda ya Mashariki ya Kati inanuia kupata uungwaji mkono wa azimio la hivi karibuni ambalo litatekelezwa kwa awamu tatu.

Mwandiplomasia huyo anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa kiutu kwa ajili ya Ukanda wa Gaza, ambao unafanyika Jordan siku ya Jumanne. Mkutano huo uliopewa jina la "Wito wa hatua: Hatua za haraka za kibinadamu kwa Gaza", umeandaliwa na Jordan, Misri na Umoja wa Mataifa.

Soma: Israel yawaokoa mateka wanne wakiwa hai huko Gaza

Utahudhuriwa na viongozi, mawaziri wa mambo ya kigeni na maafisa kutoka nchi 75 pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa ikiwemo shirika la kimataifa la msalaba mwekundu.