Biden, Ruto waahidi kulinda demokrasia Afrika na kwingineko
24 Mei 2024Ziara ya Ruto ndiyo ya kwanza ya kiserikali kufanywa na rais wa Afrika katika Ikulu ya White House tangu 2008, na inaashiria umuhimu wa bara hilo ambalo la watu bilioni 1 na lina uhusiano wa karibu wa kibiashara na China, lakini likiwa nyuma ya vita vya Ukraine na Gaza kwenye ajenda ya Washington.
Siku ya Alhamisi jioni, Ruto alikuwa mgeni rasmi katika dhifa ya chakula cha jioni iliyovutia wageni mbalimbali, kuanzia mwimbaji na mtunzi wa nyimbo Don McLean hadi kamishna wa NFL Roger Goodell, Wakurugenzi Wakuu wa Walmart na Pfizer pamoja na Rais wa zamani Bill Clinton. Rais wa zamani Barack Obama, ambaye babake alikuwa Mkenya, alijitokeza kwa muda mfupi kabla ya chakula.
"Tunaweza kutenganishwa na umbali, lakini tumeunganishwa na maadili sawa ya kidemokrasia," Biden alisema wakati akimsalimia Ruto kwenye bustani ya Ikulu. Biden alikumbusha kuhusu ziara zake mwenyewe nchini Kenya akiwa kijana, akipongeza uhusiano wa kidiplomasia wa miaka 60 kati ya nchi hizo mbili baada ya uhuru wa Kenya.
"Ziara yangu inafanyika wakati ambapo demokrasia inachukuliwa kuwa inarudi nyuma duniani kote," Ruto alisema, akiwa amesimama na Biden, Makamu wa Rais Kamala Harris na maafisa wengine wa baraza la mawaziri. Hapo awali, alikuwa amekutana kwa faragha na Biden katika Ofisi ya Oval.
"Tulikubaliana kuhusu fursa muhimu kwa Marekani kurekebisha kwa kiasi kikubwa mkakati wake na kuimarisha uungaji mkono wake kwa Afrika," Ruto alisema.
Biden alisema ataiteua Kenya kuwa nchi ya kwanza ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kuwa mshirika mkuu asiye wa NATO. Qatar, Israel na nchi nyingine 16 zinashiriki hadhi hiyo. Nairobi na Washington zinashikirikiana katika mapambano dhidi ya ugaidi barani Afrika, utulivu nchini Haiti na kuiunga mkono Ukraine.
Soma pia: Biden, Ruto kujadili msamaha wa deni kwa Kenya wiki hii
Rais huyo wa Kenya aliwasili nchini Marekani siku ya Jumatatu na kutembelea Atlanta, kisha akafanya mazungumzo na watendaji wa sekta ya biashara katika Ikulu ya White House siku ya Jumatano. Ijumaa atajadili ushirikishwaji wa kidigitali wa Afrika na Makamu wa Rais Kamala Harris katika hafla inayoandaliwa na Chama cha Wafanyabiashara wa Marekani.
Serikali za Marekani zilizofuata zimesema zilitaka kuzipa nchi za Afrika njia mbadala endelevu na mbadala ya kidemokrasia kwa uhusiano na China na Urusi, lakini Washington imeshindwa kuanzisha uhusiano wa kina.
Mazingira ya kisiasa ya bara hilo yamebadilika sana katika mwaka uliopita kutokana na misururu ya mapinduzi ya kijeshi, vita na chaguzi tete ambazo zimezipa China na Urusi ushawishi mkubwa zaidi. Biden anatumai kuimarisha uhusiano na Kenya, inayoonekana kama ngome ya kidemokrasia, inaweza kusaidia kuleta utulivu wa bara hilo na kuendeleza maslahi ya Marekani.
Katika taarifa yao ya pamoja, viongozi hao wawili walisema watashirikiana kuiunga mkono serikali ya Somalia katika mapambano yake dhidi ya ugaidi na kuzitaka pande zinazozozana nchini Sudan kuruhusu upatikanaji wa misaada ya kibinadamu na kukubaliana kusitisha mapigano.
Nishati ya kijani, makubaliano ya afya
Viongozi hao walitangaza uwekezaji mpya unaoungwa mkono na Marekani katika utengenezaji wa nishati ya kijani na afya, pamoja na mpango wa kina wa kupunguza mzigo wa madeni makubwa ya Kenya, ambayo mengi yake inadaiwa na China.
Shirika la Ufhadhili wa Maendeleo ya Kimataifa la Marekani lilitangaza dola milioni 250 za uwekezaji mpya nchini Kenya kupitia Shirika la Fedha la Kimataifa la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa. Fedha hizo zinajumuisha dola milioni 180 kwa ajili ya mradi mkubwa wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu, afisa wa serikali ya Marekani alisema, na kufanya uwekezaji wa shirika hilo la Marekani nchini Kenya kufikia zaidi ya dola bilioni 1.
Viongozi hao wawili walitoa wito wa pamoja kwa jumuiya ya kimataifa kupunguza mzigo mkubwa wa madeni wa nchi zinazoendelea na kufanya zaidi kusaidia nchi maskini zinazotaka kuwekeza katika teknolojia ya maendeleo na tabinachi. Walitoa wito pia kwa bunge la Marekani kupitisha muswada wa kurefusha makubaliano ya bishara kati ya Marekani na Afrika.
Mgogoro wa kibinadamu wa Haiti ulikuwa mada nyingine. Mpango wa Kenya wa kupeleka maafisa 1,000 wa kijeshi katika nchi hiyo ya Karibia kama sehemu ya juhudi zinazoungwa mkono na Umoja wa Mataifa za kukabiliana na ghasia za magenge na njaa umecheleweshwa, duru ziliiambia Reuters.
Siku ya Jumatano, Biden aliwaambia waandishi wa habari kuwa anapanga kuzuru Afrika mwezi Februari baada ya uchaguzi wa rais wa Marekani, tangazo ambalo linalotoa taswira kwa rais Mdemokrat atamshinda mpinzani wake wa chama cha Republican Donald Trump. Biden hapo awali aliahidi kufanya safari ya kwenda Afrika wakati fulani mnamo 2023.
Chanzo: RTRE