1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Biden, Zelenskiy wajaribu kuizuwia Congress kusitisha msaada

Hawa Bihoga
23 Desemba 2022

Ziara ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky mjini Washington wiki hii ilikuwa wakati wa ikulu ya White House kumuonyesha Rais wa Urusi Vladmir Putin kwamba Marekani itadumisha azma yake ya vita "kadiri itakavyohitajika."

https://p.dw.com/p/4LNf8
USA Ukraine Volodymyr Selenskiy bei Joe Biden, PK im Weißen Haus
Picha: Kevin Lamarque/REUTERS

Ziara hiyo pia ilimpa rais wa Ukraine, alievalia mavazi ya kijeshi ya rangi ya kijani, fursa katika uwanja mkubwa wa bunge la Congress, kuwashukuru wabunge kwa mabilioni ya dola yanayodumisha mapambano ya nchi yake.

"Kadiri itakavyochukuwa" ni kauli nzito, lakini hivi sasa inakabiliwa na swali gumu: Ni uvumilivu kiasi gani litakuwa nao bunge hilo lililogawika - na umma wa Marekani kwa vita ambavyo havina mwisho wa wazi na ambavyo vimeuathiri vibaya uchumi wa dunia?

Soma pia: Marekani, Ufaransa zaapa kuiwajibisha Urusi kwa vita Ukraine

Jumatano usiku, rais Zelensky alitoa hoja yake mbele ya mkutano wa pamoja wa mabaraza yote ya bunge la Marekani, akiunganisha mapambano ya kudumisha mamlaka ya taifa lake na vita vya Marekani vya uhuru.

Alizungumzia vita vya mji wa Bakhmut, ambako mapigano makali ya mwezi mzima mashariki mwa Ukraine yanaendelea - kama mapambano ya nchi yake ya Saratoga, ambayo ilibadili mambo wakati wa vita vya mapinduzi ya Marekani.

Zelensky, alietembelea uwanja wa mapambano mjini Bakhmut muda mfupi kabla ya kusafiri kwenda Washington, aliwapatia wajumbe wa baraza la wawakilishi bendera ya Ukraine iliyosainiwa na wanajeshi, na wakati akitoa shukrani kwa msaada wa Marekani, aliwaambia pia wabunge kwamba pesa zao siyo msaada, bali uwekezaji katika usalama wa dunia na demokrasia, ambao wanautumia kwa njia ya uwajibikaji zaidi.

USA Washington | Ankunft Ukrainischer Präsident Selenskyi
Rais Zelenskiy akitemebea na mkuu wa itifaki wa Marekani Rufus Gifford wakati akiwasili Washington kwa mazungumzo na Rais Joe Biden na kuhutubia bunge la Congress, Desemba 21, 2022.Picha: Ukrainian Presidential Press Service/REUTERS

Wamarekani waendelea kuunga mkono msaada

Utafiti wa maoni ya wanachi unaonyesha kuwa Wamarekani walio wengi wanaendelea kuunga mkono kutolewa msaada kwa Ukraine kutokana na kufanikiwa kurudisha nyuma jeshi la Urusi ambalo baadhi ya maafisa wa serikali ya Marekani waliamini awali kwamba lingevisambaratisha haraka vikosi vya Ukraine.

Soma pia: Urusi yaamuru kuondoa vikosi kutoka mji wa Ukraine wa Kherson

Lakini Waukraine wanaozidiwa idadi, kwa msaada wa kijeshi wa karibu dola bilioni 21.3, tangu uvamizi wa Februari, wameweza kusajili mafanikio kadhaa kwenye uwanja wa vita na kusababisha hasara kubwa kwa wanajeshi wa Urusi.

Zelensky, akiwa amekaa karibu na Biden katika ofisi ya rais, alikiri kuwa Ukraine ilikuwa katika nafasi nzuri kwa sababu ya uungaji mkono wa vyama vyote vinavyowakilishwa bungeni.

"Tunadhibiti hali kwa sababu ya msaada wenu", alisema Zelensky, ambaye pia alimpa Biden nishani iliyokuwa imetolewa kwa kapteni wa Ukraine anayehusika na mifumo ya roketi aina ya HIMARS iliyotolewa na Marekani, ambayo afisa huyo alitaka Biden aichukuwe.

USA Volodymyr Selenskiy spricht vor dem US Congress in Washington
Rais Volodymyr Zelenskiy akikabidhi bendera ya Ukraine iliyosainiwa na wanajeshi wanaopigana mjini Bakhmut kwa spika wa bunge la Marekani Nancy Pelosi, wakati makamu wa rais Kamala Harris akipiga makofi, wakati wa mkutano wa pamoja wa mabaraza ya bunge, Desemba 21, 2022.Picha: Jonathan Ernst/REUTERS

Na licha ya msaada kwa Ukraine kusifiwa na spika wa baraza la wawakilishi Nancy Pelosi na kiongozi wa Warepublican katika Baraza la Seneti, Mitch McConnell kama inayohudumia maslahi ya msingi ya Marekani, umoja wa vyama kuhusu Ukraine ulikuwa unaanza kupungua.

Mzozo ndani ya Republican

Muda mfupi kabla ya kuwasili kwa Zelensky, Marekani ilitangaza msaada mwingine wa dola bilioni 1.85 kwa Ukraine, ikiwemo mifumo ya ulinzi wa anga ya Patriot, na bunge lilipanga kupiga kura kuhusu mpango wa matumizi unayohusisha msaada wa ziada wa dola bilioni 45 katika msaada wa dharura kwa Ukraine.

Soma pia:Zelensky ataka ulinzi katika usafirishaji nafaka za Ukraine 

Hata hivyo, bado kulikuwapo na ishara za kutoridhika ndani ya chama cha Republican. Mwakilishi Kevin McCarthy, anayewania kuwa spika ajae wakati Warepublican watakapochukuwa udhibiti wa baraza la wawakilishi katika mwaka mpya, amesema chama chake hakitatoa uhuru usio na mipaka kwa ajili ya Ukraine mara kitakapochukua udhibiti. Baadhi ya wanachama wenye msimamo mkali zaidi ndani ya chama wamemkosoa McConnell kuhusiana na uungaji wake mkono kwa Ukraine.

Wakati mrengo mkali wa kulia unaanza kuongeza sauti kuhusu mashaka yao ya matumizi, suala la Ukraine ni rahisi kuuzika kuliko mizozo ya muda mrefu na yenye gharama kubwa, alisema Elliot Abrams, aliyehudumu katika nafasi za juu za kiusalama na mambo ya nje katika tawala za marais wa zamani Donald Trump, George W. Bush na Ronald Reagan.

Chanzo: AP