Blinken aiomba Ethiopia kuimarisha amani baada ya vita
15 Machi 2023Viongozi hao wawili wamesema hayo katika wakati ambapo pande hizo mbili zinajaribu kurejesha mahusiano ya kidiplomasia yaliyovurugwa na vita katika jimbo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia.
Anthony Blinken yuko ziarani mjini Addis Ababa na kwanza alikutana na waziri mwenzake wa mambo ya nje Demeke Mekonnen, lakini pia akitarajiwa kukutana na viongozi wa vikosi vya Tigray vilivyopambana na vikosi vya serikali katika jimbo la Tigraykatika vita vilivyodumu kwa miaka miwili.
Blinken na Abiy wamezungumzia mambo kadha wa kadha kwa kina yahusuyo Ethiopia, mataifa hayo mawili na ya kikanda yenye maslahi kwa mataifa yote mawili. Kabla ya kukutana na Abiy, Blinken alifanya mazungumzo mapana na Mekonnen na kuzungumzia kuanzia utekelezaji wa makubaliano ya kusitishwa kwa uhasama hadi hali ya kiuchumi ya taifa hilo na masuala ya amani na usalama ya kikanda.
Kupitia kwenye ukurasa wake wa twitter, Abiy ameandika kwa pamoja wamekubaliana kuimarisha makubaliano ya muda mrefu baina ya mataifa yao.
Kabla ya mkutano huo Blinken alimwaambia waziri mkuu Mekonnen kwamba bado kuna masuala mengi yanayotakiwa kufanywa, ingawa alisema la muhimu zaidi litakuwa ni kuendeleza amani katika eneo zima la kaskazini mwa Ethiopia.
Blinken amesema "Ni jambo jema kurudi Afrika, na hasa Ethiopia...nadhani katika kipindi muhimu sana, kipindi cha matumaini kutokana na amani huko eneo la kaskazini na hilo linatakiwa kuendelea, na mimi na wewe pamoja na waziri mkuu tutalizungumzia hilo na malengo yetu ya pamoja katika maeneo mengine kama tulivyosema, kwa lengo la kuimarisha uhusiano kati ya Marekani na Ethiopia. Kuna mengi ya kufanywa lakini jambo la muhimu zaidi ni amani inayoendelea eneo la kaskazini na kuimarisha uhusiano wetu tunaposonga mbele."
Maafisa wa ngazi za juu wa Marekani wakimbilia Afrika kuimarisha mahusiano dhidi ya China.
Mazungumzo hayo pia yalihusisha mjadala kuhusu kuundwa kwa serikali ya mpito katika jimbo la Tigray na sera ya kipindi cha mpito itakayohusisha uwajibikaji na haki kwa waathirika wa vita hivyo, hii ikiwa ni kulingana na wizara ya mambo ya nje ya Ethiopia kupitia mtandao wa Twitter.
Soma Zaidi: Marekani na Ethiopia wajadili uwajibikaji huko Tigray
Ikumbukwe, Marekani ilikuwa mkosoaji mkubwa wa mauaji ya kiholela yaliyofanywa na vikosi vya Ethiopia na washirika wake Eritrea na kutoka jimbo la Amhara wakati wa vita kwenye jimbo la Tigray na kuiwekea serikali hiyo vizuizi katika misaada yake ya kiuchumi na kiusalama iliyokuwapatia Ethiopia.
Lakini kama ishara ya kurejesha upya mahusiano, Blinken ametangaza hii leo msaada wa huduma za kiutu nchini humo wa dola milioni 33. Amesema msaada huo utatumika kuwasaidia watu walioathiriwa na mzozo, ukame na ukosefu wa chakula.
Ziara ya Blinken nchini Ethiopia ni ya karibuni zaidi katika mfululizo wa ziara za maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya rais Joe Biden barani Afrika, wakati Washington ikihangaika kuimarisha mahusiano na bara hilo, ambako ushawishi wa China katika nyanja za kidiplomasia na uchumi ukiwa umekita mizizi. Kesho Alhamisi atakwenda Afrika Magharibi na Niger ambako kuna changamoto kubwa ya uasi wa makundi ya Kiislamu, wakati makamu wa rais Kamala Harris akitarajiwa kutembelea Ghana, Tanzania na Zambia.