Blinken atua Saudi Arabia kwa mazungumzo
20 Machi 2024Blinken anatazamiwa kukutana kwa mazungumzo na Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman.
Hii ni ziara ya sita ya Blinken huko Mashariki ya Kati, tangu kuanza kwa vita kati ya Israel na kundi la Hamas Oktoba 7 mwaka jana.
Blinken anatarajia kuzungumza na wadau mbalimbali wa mchakato wa amani katika mzozo huo, katika juhudi za kutaka kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano, kuachiwa kwa mateka na kuongeza kasi ya uwasilishaji wa misaada katika ardhi ya Palestina.
Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant anatarajiwa pia kuelekea mjini Washington wiki ijayo, huku shinikizo likiongezeka dhidi ya Israel ambayo imetakiwa kuachana na mpango wake wa kuishambulia Rafah. Hayo yakiarifiwa, wizara ya afya inayodhibitiwa na Hamas imesema hadi sasa watu 31,923 ndio wameuawa huko Gaza.