Brazil yaapa kuilinda demokrasia
9 Januari 2023Ulinzi unaimarishwa katika mji huo wa Brasilia, wakati miito ya kulaani uvamizi uliofanywa jana Jumapili na wafuasi hao ikiendelea kutolewa na mataifa mbalimbali ulimwenguni.
Polisi waliokuwa na silaha nzito wengi wakiwa wamepanda farasi, wameonekana wakijipanga mbele ya kambi hiyo, ambako wafuasi wenye misimamo mikali ya mwanasiasa aliye na mrengo mkali wa kulia Bolsonaro walionekana wakiwa wamevalia mavazi yenye rangi ya kijani na njano yanayowakilisha bendera ya Brazil.
Katika mkasa wa kustaajabisha uliorejesha kumbukumbu ya uvamizi wa Januari 6, mwaka 2021 wa jengo la bunge nchini Marekani na wafuasi wa rais wa wakati huo Donald Trump, wafuasi wa Bolsonaro walivunja vizuizi vya polisi, madirisha na milango na kupora ofisi. Hapo awali vikosi vya usalama vilivyozidiwa vilitumia gesi ya kutoa machozi, maguruneti na maji ya kuwasha ili kupambana na wafuasi hao hadi wakawashinda.
Rais mpya wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva ambaye wakati mkasa huo ukitokea alikuwa ziarani katika mkoa wa kusini mashariki wa Araraquara uliokumbwa na mafuriko makubwa, ametia saini amri ya uingiliaji kati wa shirikisho katika mji wa Brasilia, akitoa mamlaka maalumu ya serikali yake juu ya polisi wa ndani kurejesha utulivu katika mkoa huo.
Soma Zaidi: Bolsonaro atishia kuingiza Brazil kwenye mzozo wa kikatiba
Vurugu hizo zimeendelea kulaaniwa na viongozi wa ulimwengu. Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amelaani ghasia hizo na kuonyesha mshikamno kwa serikali ya Lula da Silva. Kupitia msemaji wake Steffen Hebestreit, Scholz, amesema uvamizi huo ni shambulizi dhidi ya taasisi za demokrasia.
"Tuliziangalia kwa hofu picha za kutisha zilizotufikia jana usiku. Hili ni shambulio dhidi ya taasisi za kidemokrasia na kwa hivyo ni shambulio dhidi ya demokrasia. Tunasimama bega kwa bega na watu wa Brazil na vile vile Rais aliyechaguliwa kidemokrasia Lula da Silva. Inadhihirika wazi jinsi demokrasia inavyotakiwa kuwa na nguvu ili kujilinda dhidi ya jambo kama hili.,' amesema Hebestreit
Mamlaka zaapa kuilinda demokrasia.
Mamlaka nchini Brazil zimeapa kuilinda demokrasia na kuwawajibisha wahusika wa vurugu hizo. Mamlaka hizo zimesema zinataka kuchukua hatua kali kama ishara inayolenga kuzuia mashambulizi zaidi dhidi ya utawala wa sheria.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis mapema leo amelaani vikali kadhia hiyo aliyoielezea kama ishara ya kudhoofika kwa demokrasia katika bara la Amerika.
Papa Francis ametoa matamshi hayo kwenye hotuba yake ya kila mwaka kwa mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao mjini Vatican. Amesema, katika maeneo mengi, ishara ya kudhoofika kwa demokrasia huonekana katika ongezeko la migawanyiko ya kisiasa na kijamii. Ameigusia ia Peru, ambako kuna maandamano ya nchi nzima yaliyogubikwa na ghasia na kusababisha vifo vya watu 22, lakini pia hali ya kutia wasiwasi huko Haiti ambako magenge ya uhalifu yanazidi kuongeza mashaka kwa raia.
Ikulu ya Urusi, Kremlin imesema mapema leo kupitia msemaji wake Dmitry Peskov kwamba inamuunga mkono rais mpya wa Brazil da Silva, huku ikilaani vikali machafuko hayo ya wafuasi wa Bolsonaro.
Taarifa ya pamoja kutoka kwa mihimili mitatu ya serikali ya Brazil pia imeelezea kulaani tukio hilo waliloliita shambulizi la kigaidi. Kaimu rais wa baraza la seneti Veneziano Vital do Rego, spika wa Baraza la wawakilishi Arthur Lira na mwanasheria mkuu Rosa Weber wametia saini taarifa hiyo wakisema wameungana ili hatua za kitaasisi zichukuliwe kwa misingi ya sheria za Brazil, huku wakihimiza utulivu na amani.
Sikiliza Zaidi: