Burkina Faso yatibua jaribio la mapinduzi
24 Septemba 2024Waziri wa usalama wa Burkina Faso Mahamadou Sana amesema katika taarifa iliyosomwa kwenye televisheni ya taifa Jumatatu usiku kuwa walifanikiwa kuzuia majaribio kadhaa ya kuvuruga utulivu wa nchi hiyo.
Waziri Sana ameongeza kusema kuwa Luteni-Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba, ambaye aliondolewa madarakani mwaka 2022, ndiye aliyeongoza mpango wa kijeshi wa njama hiyo, huku watu kadhaa wakikamatwa akiwemo Ahmed Kinda, kamanda wa zamani wa kikosi maalum nchi humo.
Soma: Duru za usalama: Watu zaidi ya 70 waliuawa katika shambulio la Bamako
Damiba aliingia madarakani katika mapinduzi ya Januari mwaka 2022 yaliyomuondowa aliyekuwa rais mteule wakati huo Roch Marc Christian Kabore. Takriban miezi minane baadaye, Damiba mwenyewe alipinduliwa na kapteni Ibrahim Traore, mwenye umri wa miaka 34 na ambaye kwa sasa yuko madarakani.
Chini ya utawala wa Traore, nchi hiyo ya Afrika Magharibi isiyo na bandari ilimpa kisogo mkoloni wake wa zamani Ufaransa na kuapa kukomesha uasi wa makundi ya itikadi kali ambao ulitokea nchi jirani ya Mali mnamo mwaka 2015.
Tangu wakati huo, Burkina Faso imeigeukia Urusi kwa usaidizi wa kijeshi huku ikiimarisha uhusiano wake na mataifa ya Iran na Uturuki, pamoja na nchi za Sahel za Mali na Niger, ambazo pia zinatawaliwa na serikali za kijeshi zilizoingia madarakani kwa mapinduzi na zinazopambana pia na ghasia za makundi ya itikadi kali.
Soma pia: Burkina Faso na Mali zatangaza vita dhidi ya yeyote atakaeivamia Niger
Wataalam wanahofia kuwa Afrika Magharibi imekuwa kitovu cha ugaidi duniani hasa wakati huu majeshi ya nchi za Magharibi yakiondoka eneo hilo. Heni Nsaibia ni Mratibu katika taasisi ya kukusanya data kuhusu maeneo yenye mizozo Afrika Magharibi (ACLED).
" Na tukiangalia Mali, Burkina Faso na Niger, nchi hizi zote zinaelekea mwaka huu kuwa katika hali mbaya zaidi. Hali ya usalama inazidi kuzorota na hiyo ndiyo hali jumla. Tawala za kijeshi katika kanda hiyo, zimeyazuia mashirika yasiyo ya kiserikali na mashirika ya kibinadamu. Baadhi yao hata yamechukuliwa hatua. Na hii inajumuisha pia waangalizi kutoka Umoja wa Mataifa walioko katika nchi hizo kama Burkina Faso kwa mfano."Viongozi wa Afrika Magharibi kujadili njia za kuhakikisha usalama nchini Mali, baada ya kufika mwisho kwa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo.
Makundi yenye itakadi kali yenye mafungamano na makundi ya kigaidi ya al Qaeda au kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS yamesababisha vifo vya maelfu ya raia na huku mamilioni ya wengine wakilazimika kuyakimbia makazi yao huko Burkina Faso, Mali na Niger.