1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cameron aonya kujiondoa Umoja wa Ulaya

23 Februari 2016

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron ameonya kwamba kura ya maoni juu ya kubakia nchi yake katika Umoja wa Ulaya au la, inaweza kuhatarisha uchumi na usalama wa taifa hilo.

https://p.dw.com/p/1I0If
Picha: Getty Images/AFP/J. Tallis

Akilihutubia bunge jana, Cameron alimshambulia Meya wa jiji la London, Boris Johnson hasimu wake wa muda mrefu ambaye ametamka hadharani kwamba anaunga mkono Uingereza ijiondoe kwenye Umoja wa Ulaya, akimtuhumu kuchukua msimamo huo kwa maslahi ya kisiasa.

Meya Johnson alimtaka Cameron aelezee kwa undani namna makubaliano yaliyofikiwa Brussels, Ubelgiji wiki iliyopita yatakavyoyaleta mamlaka katika sehemu yoyote ya utungaji wa sheria kwenye bunge la Uingereza.

Hata hivyo Cameron ambaye ni kiongozi wa chama cha kihafidhina, alijibu akisema yataipa serikali mamlaka makubwa zaidi juu ya mafao, uhamiaji na uwezekano wa kuondoka kutoka kwenye umoja wa karibu kabisa.

''Kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya huenda ikatufanya kwa muda kujiona tuko huru, lakini je itatupa kweli mamlaka zaidi, ushawishi na uwezo mkubwa wa kuweza kutekeleza mambo yetu? Lakini tukiondoka kwenye Umoja wa Ulaya, je tutakuwa na mamlaka ya kuzuia biashara zetu kutobaguliwa? Hapana,'' alisema Cameron.

Cameron awahakikishia wapiga kura

Amewaambia wabunge kura ya maoni itakuwa ''uamuzi wa mwisho'' na amewahakikishia wapiga kura kwamba hali ya baadaye ya nchi hiyo itakuwa bora zaidi, ikiendelea kubakia mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Baadhi ya wachambuzi wanaamini iwapo Uingereza itajiondoa katika Umoja wa Ulaya, Johnson anaweza akawa Waziri Mkuu. Matokeo ya hivi karibuni ya utafiti wa maoni ya wapiga kura yameonyesha wingi mdogo ya wapiga kura wanaotaka kubakia kwenye umoja huo, lakini idadi kubwa bado hawajaamua kuhusu kura hiyo ya maoni iliyopangwa kufanyika Juni 23, mwaka huu.

Bendera ya Uingereza na Umoja wa Ulaya
Bendera ya Uingereza na Umoja wa UlayaPicha: Reuters/Y. Herman

Wakati huo huo, viongozi wa zaidi ya theluthi tatu ya makampuni makubwa nchini Uingereza wameonya kuwa kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya kunaweza kuuweka hatarini uchumi wa nchi hiyo na kutishia ajira.

Kwenye barua yao ya pamoja iliyochapishwa katika gazeti la leo la Times, kiasi ya viongozi 198, akiwemo Roger Carr, mwenyekiti wa BAE Systems, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya mafuta ya BP, Bob Dudley na Ron Dennis, mkuu wa McLaren, wameelezea kuuunga mkono mpango wa Cameron, kuhusu mageuzi katika Umoja wa Ulaya.

Wamesema Cameron ametekeleza ahadi zake za kuimarisha ushindani ndani ya Umoja wa Ulaya na wanaamini kwamba kujiondoa katika umoja huo, kutakwamisha uwekezaji, kuhatarisha ajira na kuuweka uchumi katika hatari. Hapo jana, Paundi ya Uingereza ilishuka thamani dhidi ya Dola ya Marekani kutokana na hofu ya matokeo ya kura ya maoni.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,RTRE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman