Chadema: Tutatumia mbinu binafsi kulinda kura zetu
25 Juni 2020Chama hicho ambacho kimedai kina matarajio ya kufanya vizuri katika matokeo ya uchaguzi wa mwezi Oktoba kimesema hakina chaguo lingine mbali ya kuwa na mbinu mbadala ya kusimamia kura zake.
Kimedai hatua hiyo inatokana na kutoiamini tume ya uchaguzi iliyopo baada ya kilio chao cha miaka mingi kutopatiwa ufumbuzi.
Katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika ambaye leo amekutana na waandishi wa habari hata hivyo hakubainisha moja kwa moja jinsi watavyoutekeleza mkakati huo.
11 wawania kuipeperusha bendera ya Chadema
Suala hilo la wapinzani kulinda kura zao ilikuwa mada iliyozua mvutano mkubwa wakati wa uchaguzi mkuu uliopita wa 2015. Nalo suala la tume huru imekuwa ajenda ya kipekee kwa vyama vya upinzani ambavyo mara zote vimekuwa vikiikosoa tume iliyopo kwa madai kuwa haitoi uwakilishi kwa washiriki wote wa uchaguzi.
Wakataziri wa zamani wa mambo ya Nje, Bernard Membe ambaye amezua mjadala mkubwa kutokana na kauli yake ya kutaka kuwania urais wa mwaka huu, ameingia katika ajenda hiyo akisisitiza pia haja ya kuwa na tume huru. Hata hivyo, serikali imekuwa ikidai kuwa tume iliyopo ni huru na imeundwa kwa mujibu wa katiba na sheria.
Chadema: Shambulizi dhidi ya Mbowe lilichochewa kisiasa
Ama kwa upande mwingine, Chadema imesisitiza tena kuwa mwenyekiti wake, Freeman Mbowe alishambuliwa kisiasa huku kikipuuza taarifa zinazotolewa kwamba kiongozi huyo hakufanyiwa shambulio lolote zaidi ya kukutwa akiwa amepata kilevi.
Chama hicho kimelitupia lawama jeshi la polisi kwa madai kwamba linajaribu kipindisha ukweli wa mambo kuhusiana na tukio hilo, lililotokea wakati wa vikao vya bunge vikiendelea.
Mbali na hilo, chama hicho ambacho hivi karibuni kilitangaza majina ya wagombea 11 waliojitokeza kuwania nafasi ya urais, kimedai kuwepo kwa viashiria kwamba jeshi hilo la polisi linajitumbukiza katika masuala ya kisiasa na hivyo kufanya uwanja wa kisiasa kushindwa kutoa uwiano sawa kwa washiriki wa uchaguzi mkuu kuchuana kwa hoja na sera.