1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chadema yakamilisha hatua ya kwanza ya uchaguzi wa mabaraza

16 Januari 2025

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema, kinakamilisha hatua yake ya kwanza ya uchaguzi wa mabaraza yake ya uongozi na hatimaye baadaye kitafikia hatua ya mwisho kuchagua mwenyekiti na wasaidizi wake.

https://p.dw.com/p/4pEue
Tanzania Dar es Salam 2024 | Mkutano wa chama cha upinzani CHADEMA
Freeman Mbowe, mwenyekiti wa Chadema akizungumza katika mkutano wa viongozi katika makao makuu ya chama hicho Dar es Salaam mnamo Disemba 10, 2024Picha: Eric Boniface/DW

Mabaraza ya vijana Bavicha na lile la wazee, Bazecha yamekalisha uchaguzi yakipata sura mpya ya viongozi na wakati huu Baraza la Wanawake Bawacha liko katika hatua ya mwisho kuchagua viongozi wake. 

Wajumbe wamefurika katika ukumbi wakiwa tayari kuchagua viongozi wa chombo hicho ambacho ushawishi wake ndani ya chama unakamata alama kubwa.

Pazia la kuchukua fomu lahitimishwa Chadema

Kukiwa tayari mabaraza ya vijana na wazee viongozi wake wamejulikana katika uchaguzi ambao uliwavutia wengi, macho sasa yanaelekezwa katika chombo hicho cha wanawake kujua nani atakuwa kinara wake.

Wafuatiliaji wa mambo wanasema yoyote anayeibuka mshindi katika mabaraza hayo matatu, anabeba nafasi kubwa ya kusukuma karata yake kwa wagombea wanaowania nafasi ya uenyekiti ambayo licha ya kuwa na wagombea watatu, lakini vigogo wawili, mwenyekiti anayetetea nafasi yake, Freeman Mbowe na makamu wake, Tundu Lissu wanaendelea kuwa gumzo katika uchaguzi huo.

Lissu atoa wito uchaguzi wa Chadema ufanyike kwa uwazi

Mnamo Alhamisi, wote wamehudhuria mkutano wa uchaguzi wa baraza la wanawake wakitoa nasaha kwa wajumbe. Mwenyekiti Mbowe alihimiza haja ya chama hicho kuendelea kulinda umoja na mshikamano, akiwataka wajumbe kutoyaporomosha mafanikio yalifikiwa na chama.

Lissu katika sehemu ya nasaha zake kwa ujumbe alitilia mkazo kile anachokiamini haja ya kukaribisha mageuzi akitaka wanachama wote kuwa na nguvu na kufaidika na maendeleo ya chama.

Kuhusu baraza la vijana Bavicha, mwanasiasa kijana Deogratius Mahinyila ndiye sasa aliyechukua jukumu la kuongoza chombo hicho baada ya kuibuka mshindi katika chaguzi zinazoendelea kufanyika.

Je, kuna mpasuko ndani ya Chadema?

Wengi wanamtizama kama mwanasiasa anayevutiwa na upande wa mwanasiasa anayeegemea mabadiliko ndani ya chama hicho na tayar ametuma ujumbe kuhusu ajenda yake kuelekea katika uchaguzi mkuu wa hapo January 21.

Suzan Lyimo ambaye wakati mmoja amewahi kuwa mbunge ndiye mwenyekiti mpya wa baraza la wazee na anaonekana kuwa karibu zaidi na upande wa mgombea uenyekiti anayetetea nafasi yake.

Mbowe: Chadema haiwezi kufa kutokana na tofauti zetu

 Hata hivyo amejizuia kujibainisha moja kwa moja katika kinyang;anyiro hicho mbali ya kusisitiza kuwa anaamini ajenda yake wakati anachukua majumu hayo mapya ni kupigania maslahi ya wazee na chama kwa jumla.

Chama tawala Tanzania chashinda kwa kishindo serikali za mitaa

Uchaguzi baraza la wanawake unaoendelea sasa ni karata pekee inayosubiriwa kujua kati ya wagombea hao wawili ni nani anapata uungwaji mkono wa moja kwa moja kuelekea katika uchaguzi.

Uchaguzi wa Chadema safari hii umekuwa mada inayozungumzwa kila uchao na kwa hatua nyingine yule atayefanikiwa kuibuka mshindi huenda akakabiliwa na mtihani mkubwa wa kurejesha umoja  ndani ya chama.