Chama cha CCM chapata Makamu Mwenyekiti mpya
18 Januari 2025Wajumbe wa mkutano mkuu maalum wa chama tawala nchini Tanzania CCM wamempitisha mwanasiasa mkongwe Stephen Masato Wasira, aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika serikali ya Tanzania kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho kwa Tanzania bara.
Wasira ametangazwa rasmi siku ya Jumamosi kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Abdulrahman Kinana, ambaye alitangaza kupumzika miezi mitano iliyopita.
Makamu huyo mpya amepitishwa kwa kura za ndio 1910 kati ya kura 1921, ushindi hiuo ni ni wa kishindo ambao unaashiria Wasira amepata asilimia 99.42 ya kura zilizopigwa katika mkutano mkuu maalum wa chama cha mapinduzi, CCM unaondelea mjini Dodoma.
Akitoa shukran katika mkutano huo baada ya kupitishwa, Wasira amesema ataendeleza kazi na falsafa ya mwenyekiti wake Samia Suluhu Hassan ya maridhiano na ameongeza kwamba sasa CCM inajipanga ili kuendelea kushika dola, Tanzania bara na pia visiwani katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo utakaofanyika mwakani.
Soma Pia: Wajumbe wa chama tawala CCM kumchagua mrithi wa Kinana
Makamu mwenyekiti mpya wa CCM amesema pia atahakikisha anasimamia umoja, amani na maendeleo.
Stephen Wasira ni miongoni mwa wanasiasa mashuhuri nchini Tanzania. Ana uzoefu wa maswala ya kisiasa wa zaidi ya miongo minne.
Makamu mwenyekiti mpya wa chama cha CCM Stephen Wasira alizaliwa mwaka 1945 katika wilaya ya Bunda mkoani Mara.
Wajumbe wa chama cha CCM, walianza kukusanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete ulioko katikati ya jiji la Dodoma siku ya Ijumaa kwa ajili ya shughuli ya kupokea taarifa za kiutendaji kutoka kwa viongozi wa chama.
Kwa kawaida, makamu mwenyekiti wa chama hicho tawala ndiye anayekuwa mwenyekiti wa kamati ya maadili ambaye moja kati ya majukumu yake ni kuwamulika makada wa chama wanaokwenda kinyume wakati wa mchaka mchaka wa kuwania nafasi mbalimbali za kuteuliwa kwenye chama wakati ambapo Tanzania inaelekea kwenye uchaguzi mkuu.
Kulikuwepo majina kadhaa yaliyochomoza vichwani mwa wachambuzi wa siasa kuhusu yule atakayerithi nafasi ya Kinana, kuwa makamu mpya mwenyekiti wa chama na sasa Makamu Mwenyekiti mpya ameshatambuliwa baada ya kuchaguliwa na wajumbe wa chama cha CCM jijini Dodoma siku ya Jumamosi 18.01.2025 ambaye ni Stephen Wasira ambaye ni mtu mwenye ushawishi mkubwa ndani ya chama na hata nje.
Mkutano huo maalum wa siku mbili unafanyika kwenye makao makuu ya chama na serikali mkoani Dodoma.