1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano mkuu maalum wa chama cha CCM waanza Dodoma

18 Januari 2025

Chama tawala nchini Tanzania cha CCM leo Jumamosi kinafanya mkutano wake mkuu maalumu ambao pamoja na mambo mengine utamchagua makamu mwenyekiti wa chama hicho, Tanzania Bara.

https://p.dw.com/p/4pJfn
 Samia Suluhu Hassan |Rais wa Tansania
Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Picha: Daniel Pier/NurPhoto/picture alliance

Chama tawala nchini Tanzania cha CCM leo Jumamosi kinafanya mkutano wake mkuu maalumu ambao pamoja na mambo mengine utamchagua makamu mwenyekiti wa chama hicho, Tanzania Bara kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Abdulrahman Kinana aliyeondoka katika nafasi hiyo.

Tayari mwenyekiti wa chama hicho rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amefungua mkutano huo na kutoa hotuba katika mkutano mkuu maalum wa CCM katika ukumbi wa Jakaya Kikwete ulioko katikati ya jiji la Dodoma. Pamoja na masuala mengine Rais Samia ametoa onyo kwa baadhi ya wabunge wa chama hicho ambao tayari wameanza kampeni za kwenda majimboni kufanya vikao vya kutaka kugombea kabla ya wakati.

Soma zaidi. Wajumbe wa chama tawala CCM kumchagua mrithi wa Kinana

Shughuli kubwa katika mkutano huo ni kupokea taarifa za kiutendaji kutoka kwa viongozi wa chama hicho kabla ya kuanza kwa mchakato wa kumpata mrithi wa Kinana.

Mkutano huo maalum wa siku mbili unaofanyika kwenye makao makuu ya chama na serikali mkoani Dodoma na unamulikwa na wengi hasa kwa kuzingatia kwamba huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu wa rais na wabunge nchini Tanzania.