Chapo aahidi kuiunganisha Msumbiji
16 Januari 2025
"Mimi, Daniel Francisco Chapo, ninaapa kuiheshimu na kuhakikisha kuheshimiwa kwa Katiba, kutimiza majukumu yangu kwa uaminifu kwa ofisi ya Rais ya Msumbiji, kujitolea kwa nguvu zangu zote kulinda, kushajiisha na kuimarisha umoja wa kitaifa, haki za binaadamu, demokrasia, na ustawi wa watu wa Msumbiji na kuhakikisha haki kwa raia wote." Alisema rais huyo mpya wa Msumbiji wakati akila kiapo cha kuanza rasmi majukumu yake ya urais hapo siku ya Jumatano (Januari 16).
Chapo alikula kiapo mbele ya Rais wa Mahakama ya Katiba, Jaji Lucia Ribeiro, rais aliyemaliza muda wake, Fillipe Nyusi na mkewe, Gueta Chapo, katika uwanja uliojaa maelfu ya wafuasi wake.
Mbali na hao, walikuwepo marais kutoka Afrika, akiwemo Umar Sissoco Embalo wa Guinea Bissau na Cyril Ramaphosa wa taifa jirani la Afrika Kusini.
Soma zaidi: Baraza la katiba laidhinisha matokeo ya uchaguzi Msumbiji
Nje ya uwanja huo, maelfu ya wafuasi wa upinzani walikabiliwa tena na ukandamizaji wa vyombo vya dola, ambapo kwa mujibu wa shirika moja la kiraia, watu saba waliuawa, na hivyo kuifanya idadi ya watu waliouawa tangu maandamano yalipoanza mnamo Oktoba 9 kufikia 300.
Upinzani bado unashikilia kwamba chama tawala cha Frelimo ambacho kimekuwapo madarakani tangu kumalizika kwa ukoloni wa Kireno mwaka 1975, kiliiba uchaguzi huo uliompa ushindi wa asilimia 65 Chapo.
Uchaguzi huo umetajwa na waangalizi wa Kimagharibi kutokuwa huru wala wa haki, madai yanayokanushwa na Frelimo.
Mondlane yuko tayari kwa majadiliano
Kiongozi wa upinzani, Venancio Mondlane, ambaye alitangazwa kupata asilimia 24 na Tume ya Uchaguzi, na kurejea nchini Msumbiji wiki iliyopita baada ya miezi kadhaa ya kujificha nje ya nchi, alisema yuko tayari kwa mazungumzo na Chapo.
"Kama ni majadiliano, mimi nipo tayari," alisema.
Hata hivyo, wafuasi wake wanaendelea kushikilia kile wanachokiita ushindi wao.
Soma zaidi: Msumbiji yamuapisha rais mpya baada ya machafuko mabaya ya baada ya uchaguzi
"Kwa sasa, tuna marais wawili. Hatutaukubali utawala huu; kuna utawala wenye rais wake na kuna rais wa watu, Venancio Mondlane; kuna pia raia wa silaha, kama unavyoona, polisi, mbwa, mabomu ya machozi, ya kuwafukuza watu hapa. Wako wapi watu waliomchaguwa rais? Wapo hapa lakini wanafukuzwa." Alisema mmoja wa waandamanaji.
Wimbi la maandamano na ukandamizaji mkali kabisa wa vyombo vya usalama kufuatia uchaguzi yameshauwa watu 300 hadi sasa, wakiwemo watoto, kwa mujibu wa mashirika ya haki za binaadamu ya ndani na ya kimataifa.
Rais huyo mpya anakabiliwa sasa na kibarua kigumu cha kuituliza nchi hiyo inayopambana na makundi yenye silaha katika jimbo la Capo Delgado, na ambayo hivi karibuni imekumbwa na vimbunga kadhaa.