China: Mradi wa ujenzi wa miundombinu wapaswa kuwa bayana
26 Aprili 2019Rais Xi amesema hayo wakati wa kuufungua mkutano mjini Beijing na kwamba lengo la China ni kuimarisha ushirikiano duniani. Katika hotuba yake ya ufunguzi rais Xi amesema kuwa mradi huo wa miundombinu una lengo la kuchangia katika kuleta viwango bora vya ustawi kwa nchi zote duniani zinazoshiriki katika mradi huo. Amesema ufisadi hautavumiliwa katika mpango huo wa kujenga miundombinu ya kuyaungansiha mabara ya Asia, Ulaya na Afrika.
Mkutano huo wa mjini Beijing unahuhduriwa na viongozi zaidi ya 40 kutoka duniani kote. Waziri wa Fedha wa Uingereza, Philip Hammond amesema nchi yake ni mshiriki halisi katika mradi wa ujenzi wa miundo mbinu unaotekelezwa na China licha ya tofauti baina ya nchi mbili hizo katika masuala fulani.
Nchi zinazoendelea zinaunga mkono mradi wa miundombinu wa ujenzi wa barabara, bandari na njia za reli kwa lengo la kukuza biashara. Hata hivyo baadhi ya nchi zinang'ang'ana kulipa mikopo inayotolewa na China.
Wakati huo huo, raisXi Jinping amekutana na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na amesema kwamba kasi ya sera ya uchumi wa dunia utandawazi haitarudi nyuma na kwamba njia ya ushirikiano wa manufaa ya pande zote ndiyo sahihi ya kuifuata.
Rais Xi amesema China inatekeleza sera ya ushirikiano wa wote katika msingi wa mfumo wa kimataifa unaozingatia malengo ya Umoja wa Mataifa. Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ametilia maanani aliyosema rais Xi katika hotuba yake ya ufunguzi, hususan alipofafanua mwambatano thabiti baina ya mradi wa ujenzi wa miundombinu na ajenda ya maendeleo ya dunia.
Katibu mkuu ameeleza kuwa mradi wa ujenzi wa miundombinu unaende sambamba na ajenda ya Umoja wa Mataifa ya kuleta maendeleo endelevu hadi mwaka 2030. Amezitaka nchi zote ziitumie fursa ya mradi huo kwa munufaa wa kila upande.
Guterres anayehudhuria mkutano wa mjini Beijing amesema mradi huo wa ujenzi wa miundo mbinu unaweza kusaidia katika kuleta juhudi za kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi na kwamba una uhusiano wa karibu na ajenda ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa kufikia mwaka 2030 na Mkataba wa Paris. Guterres amesema nchi zote zinapaswa kutumia fursa inayoletwa na mpango huo ili kufanikisha manufaa ya pamoja.
Vyanzo:/RTRE/AP